" SHINYANGA YAADHIMISHA SIKU YA FAMILIA JAMII YATAKIWA KUWA MBELE KATIKA MALEZI YA WATOTO ILI KUJENGA TAIFA IMARA

SHINYANGA YAADHIMISHA SIKU YA FAMILIA JAMII YATAKIWA KUWA MBELE KATIKA MALEZI YA WATOTO ILI KUJENGA TAIFA IMARA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamoga, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi, ametoa wito kwa jamii kuwekeza kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto ili kujenga msingi imara wa familia na taifa kwa ujumla.

Lyamoga ametoa kauli hiyo leo Mei 15, 2025, katika mdahalo ulioandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia, ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kutafakari nafasi ya familia katika ustawi wa jamii.

“Nichukue fursa hii ya kipekee kuwashukuru waandaaji wa kongamano hili muhimu la kujadili masuala ya malezi na familia. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘Mtoto ni Malezi: Msingi wa Familia Bora Taifa Imara’, ikitukumbusha kwamba tusipojenga misingi bora ya familia kupitia malezi mazuri ya watoto wetu, hatuwezi kuwa na taifa imara,” amesema Lyamoga.

Ameongeza kuwa serikali kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) imejikita katika maeneo matano muhimu: afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali, na ulinzi na usalama.

Lyamoga amesisitiza kuwa changamoto nyingi zinazolikumba taifa zikiwemo mmomonyoko wa maadili na ukatili dhidi ya watoto zinatokana na udhaifu wa malezi kuanzia ngazi ya familia. “Ni matumaini yangu maazimio yatakayopatikana hapa yatawasilishwa serikalini na pia kuingia kwenye kongamano la kitaifa la Malezi Summit Mei 23-24 mwaka huu,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile amewakumbusha wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata malezi bora ili taifa lipate kizazi chenye maadili na afya njema.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa, Lydia Kwesigabo, ametaja baadhi ya maazimio ya mdahalo huo kuwa ni:kuwe na uendelevu wa midahalo kuhusu masuala ya malezi, Kuendelea kutoa elimu kwa jamii, wazazi na walezi kuhusu malezi ya watoto,Kufikisha elimu hiyo hadi katika vyuo mbalimbali.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa, Christina Gunje, amekemea vikali mmomonyoko wa maadili unaoanzia katika familia ambapo amesema familia nyingi hazina utaratibu wa kuzungumza na watoto wao, hali inayochangia watoto kukosa maarifa sahihi ya maisha.

Gunje ameonya pia juu ya ukatili wa watoto kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa wazazi wawe makini na matumizi ya teknolojia kwa watoto.

Baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wamechangia maoni mbalimbali kuhusu njia bora za kuimarisha malezi, wakisisitiza elimu ya mara kwa mara kwa wazazi na ushirikishwaji wa jamii kwa ujumla.

Mdahalo huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, wataalamu wa afya, elimu na ustawi wa jamii.

Mdahalo huo umehudhuriwa na wawakilishi kutoka: Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga, Kamati ya Amani ya Mkoa, Viongozi wa dini, Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Mitaa wa Manispaa ya Shinyanga, Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), Waandishi wa masuala ya malezi kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa, Shirika la ICS linalojihusisha na malezi ya watoto, Mitandao ya SHY EVAWC, SMAUJATA na Chama cha Wanaume Mkoa, Umoja wa vituo vya malezi ya watoto wadogo na makao ya watoto, Baraza la Wazee Mkoa na Baraza la Watoto Mkoa, Wawakilishi wa watu wenye ulemavu, vijana, wanawake na watoa huduma ngazi ya jamii kupitia shirika la Justwai, Wanafunzi kutoka vyuo vya Serikali za Mitaa – Hombolo na SHYCOM.

 

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamoga, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamoga, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa, Lydia Kwesigabo.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa, Christina Gunje.





Post a Comment

Previous Post Next Post