" MSIJIHUSISHE NA RUSHWA - NHAMANILO

MSIJIHUSISHE NA RUSHWA - NHAMANILO


Na Mwandishi wetu –SHINYANGA

Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake  Tanzania U.W.T CCM  Wilaya ya Shinyanga Mjini  Bi Rehema Nhamanilo ameonya wanachama wa  jumuiya hiyo  kuepuka kupokea zawadi  za watia nia wa nafasi za Ubunge na udiwani kwa lengo la kuwachagua  kwenye  uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu 2025,kwani amesema kwa kufanya hivyo ni kuhalalisha rushwa.

Nhamanilo ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM na jumuiya zake katika kata za Mwamalili,Old Shinyanga,Kizumbi,Ibinzamata na Ibadakuli ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kamati ya utekelezaji ya U.W.T Wilaya ya Shinyanga Mjini,ambayo imelenga kukagua uhai wa Chama.

Amesisitiza viongozi na wanachama kuepuka kupokea zawadi za watia nia wa  nafasi za uongozi kwenye uchaguzi Mkuu baadaye Mwaka huu,na badala yake wanapaswa kuwa mfano na kielelezo cha uadilifu kwa kuzingatia miiko ya chama hicho,na kuongeza kuwa kwa kushiriki vitendo hivyo inachangia kurudisha nyuma maendeleo.

Amekemea  pia kuhusu tabia ya kuchafuana na kudhoofishana kisiasa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais,wabunge na madiwani,na badala yake waendelee kushirikiana na kuimarisha  umoja na mshikamano miongoni mwao,kwani ndiyo silaha ya ushindi.

Ametahadharisha kuepuka kampeini kabla ya wakati kwani kwa kufanya hivyo ni fujo na ukiukaji wa  maadili ya Chama lakini pia ni kuwakatisha tamaa na kuwadhoofisha kisaikolojia wabuge na madiwani waliopo madarakani,ambapo ametaka waachwe wakamilishe kipindi chao kilichobaki, na amesisitiza kuhusu misingi ya utu,heshima na ubinaadamu,”waacheni wafanye kazi,wakamilishe kipindi chao kilichobaki,msiwabeze  viongozi waliopo madarakani,wasipuuzwe, subirini wakati wa kampeini utakapofika kuliko kuanza sasa”

Mwenyekiti huyo wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini amesema wakati utakapofika wanachama hao hasa wanawake  wachukue  fomu za kugombea ubunge na udiwani,kwani hiyo ndiyo demokrasia.

Kwa upande wake katibu wa UWT –CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Bi Getrude Mboyi amewakumbusha viongozi wa kata na matawi kuwajibikia jukumu la kusimamia uhai wa chama na wanachama kuhakikisha  wanalipa  ada ili kuendelea kuimarisha uimara wa CCM na jumuiya zake.

 Katika ziara hiyo wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT wilaya ya Shinyanga Mjini wamewasilisha mada za maadili na uchaguzi,ukatili wa kijinsia,mahusiano na  ushirikiano na jamii.

Ziara hiyo iliyoanza tangu Mei 12,2025 inatarajiwa kuhitimishwa Mei 19,2025 ambapo viongozi hao wa UWT wilaya ya Shinyanga  mjini watatembelea katika kata zote, na tayari viongozi hao wamekwishatembelea kata za Ibadakuli,Kizumbi,Ibinzamata,Mwamalili na Old Shinyanga ambapo leo Mei 15,2025  walikuwa  Chibe  na Lubaga.MWISHO



 

Post a Comment

Previous Post Next Post