" KANISA LA DELIVER HOPE CHURCH OF ALL NATIONS LATAMATISHA MFUNGO WA SIKU 38 KUOMBEA UCHAGUZI MKUU 2025

Top News

KANISA LA DELIVER HOPE CHURCH OF ALL NATIONS LATAMATISHA MFUNGO WA SIKU 38 KUOMBEA UCHAGUZI MKUU 2025

Askofu Ayubu Mwakibinga akiongoza waumini wa Deliver Hope Church of All Nations katika maombi maalumu ya mfungo wa siku 38 kuliombea amani ya Taifa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, uliofanyika katika makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Kijiji cha Nyanende, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, Kanisa la Deliver Hope Church of All Nations limetamatisha rasmi mfungo na maombi ya siku 38 yaliyoanza tarehe 1 Agosti 2025 kwa lengo la kuliombea Taifa la Tanzania kuelekea uchaguzi huo.

Akizungumza mgeni rasmi, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Richard Makoye, amepongeza Deliver Hope Church of All Nations kwa kujitolea kuandaa mfungo huo muhimu kwa Taifa huku akisema kuwa  Serikali inatambua na kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kudumisha amani, mshikamano na utulivu, hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

"Maombi yenu yana mchango mkubwa katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na utulivu. Serikali inatambua mchango wa makanisa na taasisi zote za dini katika kudumisha mshikamano wa kitaifa. Nitoe wito kwa viongozi wa dini na wananchi wote kuendelea kuombea nchi yetu, ili tupate viongozi wenye maono ya kweli, moyo wa kulitumikia Taifa na kuwaletea maendeleo wananchi," amesema Makoye.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha inasimamia uchaguzi kwa uadilifu, uwazi na haki, huku akihimiza wananchi wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi.

Maombi hayo yalifanyika katika makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Kijiji cha Nyanende, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, chini ya uongozi wa Askofu na Mwasisi wa Kanisa hilo, Ayubu Mwakibinga, ambaye amesisitiza kuwa maombi hayo yamelenga hasa kuombea amani ya Taifa, mshikamano wa kitaifa na upatikanaji wa viongozi waadilifu watakaochaguliwa kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Askofu Ayubu Mwakibinga amesema maombi hayo hayakulenga tu kuliombea uchaguzi, bali pia kuombea umoja wa kitaifa, kuondoa migawanyiko ya kisiasa na kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kubaki kuwa kisiwa cha amani barani Afrika.

Askofu huyo pia amewaasa viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya Taifa na siyo maslahi binafsi au ya vyama vyao, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushiriki kwa amani katika michakato yote ya uchaguzi.

Baadhi ya waumini waliohudhuria maombi hayo, akiwemo Bi. Restuta Julius na Ndg. Mussa Ayubu, wameeleza furaha yao kwa namna kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele kuliombea Taifa ambapo wamesema maombi hayo yamewajenga kiroho na kuimarisha mshikamano wao kama waumini na wananchi wa Taifa la Tanzania.

Mfungo huu wa siku 38 umekuwa sehemu ya maandalizi ya kiroho kuelekea uchaguzi mkuu, ikiwa ni ishara ya mshikamano kati ya waumini na viongozi wa dini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani, upendo na maendeleo endelevu.

Askofu Ayubu Mwakibinga akiongoza waumini wa Deliver Hope Church of All Nations katika maombi maalumu ya mfungo wa siku 38 kuliombea amani ya Taifa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, uliofanyika katika makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Kijiji cha Nyanende, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga.

Mgeni rasmi, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Richard Makoye, akihutubia waumini na wageni waalikwa katika kilele cha maombi ya mfungo wa siku 38 yaliyoandaliwa na Deliver Hope Church of All Nations kwa ajili ya kuliombea amani ya Taifa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, uliofanyika katika Kijiji cha Nyanende, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga.

Post a Comment

Previous Post Next Post