" WANANCHI WA SHINYANGA WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA ZA MACHO KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA

WANANCHI WA SHINYANGA WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA ZA MACHO KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wenye changamoto ya magonjwa ya macho wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya macho zitakazoanza kutolewa rasmi kuanzia Juni 2, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Huduma hiyo mpya inalenga kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaosafiri umbali mrefu kufuata matibabu ya macho katika hospitali kubwa kama Bugando Mwanza au Muhimbili Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Luzila John amesema huduma hiyo ya macho ni ya kibingwa na itakuwa ikitolewa mara mbili kwa wiki katika hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa macho, uchunguzi wa kina wa macho, matibabu ya mtoto wa jicho, presha ya macho, aleji pamoja na uoni hafifu.

Amesema kuwa huduma hiyo itazinduliwa rasmi Juni 2, na siku hiyo itaambatana na kuanza kwa kambi maalum ya huduma za macho kwa wananchi ambayo itaendelea hadi Juni 6, kabla ya huduma hizo kuendelea kutolewa kwa utaratibu wa kawaida kila wiki.

Ameeleza kuwa sababu kubwa ya kuanzishwa kwa huduma hizo ni ongezeko la mahitaji ya huduma ya macho katika mkoa wa Shinyanga, ambapo awali kulikuwa na kituo kimoja tu kilichokuwa kikitoa huduma hiyo kwa kiwango kidogo.

Aidha, Dkt. Luzila amesema hospitali hiyo tayari imewekeza zaidi ya shilingi milioni 79 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vinavyotumika katika matibabu ya macho, na kwamba tayari wameshamaliza kumsomesha daktari bingwa wa macho ambaye sasa yupo tayari kuhudumia wananchi.

Baadhi ya wakazi wa Shinyanga wamepongeza kuanzishwa kwa huduma hizo wakisema kuwa hatua hiyo ni ya muhimu sana kwa sababu itapunguza gharama walizokuwa wakitumia kusafiri hadi Mwanza au Dar es Salaam kutafuta huduma za macho.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inatarajia kuwa kituo muhimu cha huduma bora kwa wagonjwa wa macho kutoka wilaya zote za mkoa huo na maeneo jirani, huku ikisisitiza kuwa huduma hizo ni endelevu, kwa kutumia wataalamu waliobobea na vifaa tiba vya kisasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post