Na: Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Katika kuhakikisha waombaji wa mikopo ya elimu wenye sifa za msingi hasa wanaotoka katika mazingira magumu wanapewa kipaumbele, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imezitaka taasisi na mashirika yanayotoa ufadhili kwa wanafunzi wa ngazi za elimu ya Sekondari na Stashahada kujisajili katika mfumo wa HESLB ili watambuliwe.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, ambapo amesema baadhi ya taasisi na mashirika yanafadhili wanafunzi lakini hawatambuliwi na HESLB, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi waliosomeshwa na taasisi hizo wanapofikia ngazi ya kuomba mikopo ya elimu, hujikuta wakikosa kipaumbele kwa sababu taasisi na mashirika yaliyowasomesha hayatambuliwi na HESLB.
"Nazihimiza taasisi na mashirika ambayo yanawasomesha wanafunzi wa Sekondari na Stashahada wajisajili katika mfumo wetu ili mifumo yetu isomane na kuondoka malalamiko ya waombaji wenye sifa hasa za kupewa kipaumbele kutokana na changamoto za kiuchumi kukosa mikopo ya elimu," amesema Dk. Kiwia.
Kwa mujibu wa miongozo ya utoaji mikopo, wanafunzi wanaotoka mazingira magumu ambao wanasomeshwa na taasisi na mashirika mbalimbali hupewa kipaumbele katika upangaji wa mikopo.
Sanjari na hilo, Dk. Kiwia ametaja faida ya usajili wa taasisi hizo kuwa utawezesha kubadilisha taarifa muhimu za waombaji, hali itakayorahisisha upangaji mikopo kwa waombaji waliosomeshwa na taasisi na mashirika hayo, kwani wengi wanatoka familia zenye mazingira magumu kiuchumi huku wengine wakiwa yatima ambapo wanapaswa kupewa kipaumbele ili waweze kutimiza ndoto zao za kupata elimu.
Taasisi na mashirika yanayotoa ufadhili kwa wanafunzi wameelekezwa kutembelea tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) ili kukamilisha usajili wao. Ikumbukwe kuwa Juni 15, 2025, HESLB ilifungua dirisha la uombaji mikopo ambapo dirisha hilo litafungwa Agosti 31, 2025, huku wito ukitolewa kwa waombaji mikopo wote kusoma na kuzingatia miongozo ya uombaji mikopo na ruzuku kabla ya kuomba mikopo hiyo.
Post a Comment