

Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa
Shinyanga, Bi. Nabila Kisendi, amewataka viongozi
wa jumuiya hiyo katika Halmashauri zote za wilaya na mkoa kwa ujumla kuendelea
kutoa elimu ya kupinga ukatili wa aina zote katika jamii wanazoishi.
Akizungumza leo
Juni 26, 2025, kwenye kikao cha ndani kilichowakutanisha wenyeviti na makatibu
wa wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga, Bi. Kisendi amesema kuwa huu ni wakati
muhimu kwa viongozi wa SMAUJATA kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya ukatili
kupitia mikutano ya hadhara, shule na taasisi za umma.
“Elimu ya ukatili haipaswi kuishia kwenye makongamano
ya kitaifa pekee, bali inapaswa kushuka hadi ngazi ya familia. Kila kiongozi ni
balozi wa mabadiliko katika eneo lake,”
amesema Bi. Kisendi.
Amesisitiza kuwa
jamii ya sasa inakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii ikiwemo ukatili wa
kijinsia, ndoa za utotoni, unyanyasaji wa watoto na wazee, hivyo ni jukumu la
viongozi wa SMAUJATA kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha umma na kuhamasisha
mabadiliko ya kitabia.
Katika kikao hicho,
viongozi wamekubaliana kubuni miradi ya kiuchumi itakayosaidia kuwawezesha
wanachama wa SMAUJATA kujitegemea kifedha, sambamba na kusaidia jamii.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kila mwanachama anapaswa kuwa tayari kushiriki
katika utekelezaji wa miradi hiyo, ili kuifanya jumuiya hiyo kuwa imara
kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake
Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, amesema kuwa jumuiya hiyo itaendelea
kushirikiana na taasisi za serikali, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
katika kuelekea kipindi cha uchaguzi, kuhakikisha rushwa haitumiki
kuwarubuni wananchi.
“Tunawahimiza wananchi kutoa taarifa za viashiria
vyote vya rushwa. SMAUJATA tutasimama bega kwa bega na TAKUKURU kuhakikisha
uchaguzi unakuwa huru na haki,”
amesema Kapaya.
Kapaya
ameongeza kuwa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Geita,
Simiyu, Mara na Kagera, inapaswa kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii
kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili bila kuchoka.
Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, George
Ntemi, amesema kuwa jumuiya hiyo itaendelea kushikamana katika mapambano dhidi
ya vitendo vyote vya ukatili vinavyoshamiri kwenye jamii.
Amesema maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho
cha viongozi wa wilaya zote yatafanyiwa kazi kwa vitendo, huku akisisitiza kuwa
SMAUJATA Shinyanga iko tayari kuyasimamia kwa nguvu zote ili kuhakikisha jamii
inapata uelewa na kinga dhidi ya ukatili.
Aidha, Ntemi amewahimiza wanachama wote wa SMAUJATA
ndani ya mkoa wa Shinyanga kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za
jumuiya hiyo, zikiwemo kampeni za uelimishaji na utekelezaji wa miradi ya
pamoja. Viongozi na taasisi za serikali pia wameombwa kuendelea kushirikiana
kwa karibu na SMAUJATA ili kuongeza ufanisi katika kufikia lengo la jamii isiyo
na ukatili.
SMAUJATA ni jumuiya inayotekeleza majukumu
yake chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum, na imekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili na
kuhamasisha haki na usawa katika jamii ya Watanzania.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo
na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga, Bi.
Nabila Kisendi, akitoe maelekezo kwenye kikao cha leo Juni 26,
2025.
Katibu
wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana
Daniel Kapaya, akizungumza
kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.
Katibu
wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana
Daniel Kapaya, akizungumza
kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.
Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mzee Mwarabu Akim, akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mzee Mwarabu Akim, akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.

Mwenyekiti wa idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Solomon Najulwa (Cheupe), akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.

Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Bunju Mkoa wa Pwani, Fathiya Issa Abdallah akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.







Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, George
Ntemi, akizungumza kwenye kikao hicho leo Alhamis Juni 26, 2025.



Post a Comment