Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Jadi la Sungusungu Wilaya ya Shinyanga
Vijijini leo Juni 12, 2025 limeadhimisha
miaka 43 tangu kuanzishwa kwake kwa sherehe iliyoambatana na ujumbe wa
kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha ulinzi wa watu na mali unaimarika
zaidi katika vijiji.
Maadhimisho hayo
yamefanyika katika Kata ya Iselamagazi yakihudhuriwa na sungusungu kutoka
tarafa tatu za Iselemagazi Mashariki, Nhindo Magharibi na Itwangi, wakiongozwa
na viongozi wao wa ngazi mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga
mgeni rasmi, Mtendaji wa Kata ya Iselamagazi Amos
Chacha, amepongeza jeshi hilo la jadi kwa kuendelea kuwa chombo
muhimu katika suala la ulinzi wa raia na mali, na kuwasisitiza wanajeshi hao wa
jadi kuendelea kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi.
"Nipende
kuwapongeza sungusungu kwa kuandaa sherehe hii ya kuadhimisha miaka 43 ya
sungusungu nawapongeza sana, kazi ya sungusungu ni kulinda mali na raia, kwenye
hili suala la ulinzi tujitahidi kuzingatia sheria na kanuni za nchi, tusije
tukajichukulia sheria mkononi," amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Sungusungu Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mabeja Halawa, amesema jeshi hilo liliundwa
kwa lengo mahsusi la kusimamia haki za watu na mali zao, likiwa chombo cha
wananchi wenyewe kwa ajili ya usalama wao.
"Jeshi la
jadi la sungusungu litaendelea kushirikiana bega kwa bega na serikali
kuhakikisha ulinzi wa watu na mali zao unaimarika zaidi vijijini,"
amesema Halawa.
Naye Mkuu wa Kituo cha
Polisi Ndindo, Blighton Rutajama, ametumia
nafasi hiyo kuwataka sungusungu kuendeleza ulinzi shirikishi kwa kushirikiana
kwa karibu zaidi na Jeshi la Polisi katika kudhibiti na kutokomeza vitendo vya
uhalifu.
Mhasibu wa Sungusungu
Wilaya hiyo Mzee Malongo Mshali akisoma historia amesema sungusungu imeanzishwa
rasmi tarehe 12 Juni, 1981, chini ya
usimamizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga iliyokuwa chini
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Mshali ameeleza
kuwa mwaka 1982, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, aliridhia rasmi Jeshi la Jadi kuwa
sehemu ya ulinzi katika jamii kwa lengo la kukabiliana na uhalifu na kulinda
mali za wananchi.
Katika sherehe hizo, kanuni
rasmi za usalama na muundo wa kamati ya ulinzi ya jadi
zimesomwa na Daud Ludelengeja, akifafanua
kuwa sungusungu huongozwa kwa misingi ya uwazi, ukweli, na nidhamu ya hali ya
juu. Mtu anayetaka kuwa kiongozi wa sungusungu anatakiwa kuwa na sifa ya kuwa
na mji, kaya, tabia njema na awe msiri na mkweli mbele ya jamii.
Muundo wa uongozi wa sungusungu unaanza na kuchagua Mtemi Mkuu, Kamanda Mkuu,
Katibu Mkuu, pamoja na makamanda wa
vikosi vidogo na wajumbe kutoka pande mbalimbali. Kiongozi hawezi kuondolewa
isipokuwa kwa sababu za kiafya, kifo, kuhama, au kuonekana na tabia mbaya mbele
ya jamii.

Mwenyekiti wa Sungusungu Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mabeja Halawa, akizungumza leo Juni 12, 2025 wakati wa sherehe ya Miaka 43 tangu kuanzishwa wa Sungusungu.

Mwenyekiti wa Sungusungu Wilaya
ya Shinyanga Vijijini, Mabeja Halawa, akizungumza leo Juni 12, 2025 wakati wa
sherehe ya Miaka 43 tangu kuanzishwa wa Sungusungu.

Mgeni rasmi, Mtendaji wa Kata ya Iselamagazi Amos Chacha, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, kwenye maadhimishi ya Miaka 43 ya Susungu Wilaya ya Shinyanga vijijini leo Juni 12, 2025.

Mgeni rasmi, Mtendaji wa Kata ya Iselamagazi Amos Chacha, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga, kwenye maadhimishi ya Miaka 43 ya Susungu Wilaya ya Shinyanga
vijijini leo Juni 12, 2025.
Mhasibu wa Sungusungu Wilaya hiyo Mzee Malongo Mshali akisoma historia ya jeshi hilo la jadi.


Mkuu wa Kituo cha Polisi Ndindo, Blighton Rutajama, akizungumza kwenye maadhimishi hayo ya
Miaka 43 tangu kuanzishwa kwa jeshi la jadi Sungusungu Wilaya ya Shinyanga
vijijini.
Post a Comment