" JUKWAA LA MWAKA LA ASASI ZA KIRAIA WILAYA YA KAHAMA LAFANYIKA, WADAU WATOA ELIMU

JUKWAA LA MWAKA LA ASASI ZA KIRAIA WILAYA YA KAHAMA LAFANYIKA, WADAU WATOA ELIMU


 
Afisa Maendeleo ya jamii wa Mkoa wa Shinyanga Bestina Gunja, akizungumza

Jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga limefanyika na kuwakutanisha mashirika zaidi ya 40 pamoja na wadau mbalimbali.

Jukwaa hilo limefanyika June 19 katika ukumbi wa askofu manispaa ya Kahama, kwa lengo la kufanya tathmini ya michango ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa jukwaa hilo, mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Shinyanga Bakari Juma amesema jukwaa hilo limewawezesha washiriki Pamoja na wadau waliohudhuria kutoa mada mbalimbali zilizolenga kuyaimarisha mashirika.

Amesema moja ya changamoto za mashirika hay ani masuala ya kikodi kwao, ambapo ata hivyo elimu imetolewa na washiriki wakapata nafasi ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu huku akiendelea kuyasihi mashirika kuendelea kufuata miongozo na taratibu za uendeshaji wa mashirika hayo.

“Kama ambavyo tunafahamu kuna changamoto ya maswala ya kikodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, TRA imetoa elimu na kuelezea sheria inasema nini, washiriki wameuliza maswali kwa hiyo tumepata uelewa” Amesema Bakari


Miongoni mwa wadau waliohudhuria jukwaa hilo ni Pamoja na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU, Mamlaka ya mapato Tanzania TRA, Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF), Ofisi ya maendeleo ya jamii wilaya na mkoa pamoja, wamiliki pamoja na viongozi wa asasi za kiraia kutoka ndani na nje ya wilaya ya Kahama ambapo wadau walipata nafasi ya kutoa elimu kwa washiriki hao.

Akizungumza pembezoni mwa jukwaa hilo, ofisa maendeleo ya jamii kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bestina Gunja amesema utendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo ni mzuri na kuyataka mashirika bubu machache yanayojaribu kutaka kuharibu taswira ya mashirika, kuhakikisha yanafuata sheria na taratibu za uanzishaji wake.

Gunja ameyahimiza mashirika yote yanayotekeleza shughuli zake ndani ya mkoa huo, wahusika wake wahakikishe wanafika ofisi ya mkuu wa mkoa kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yake kwa ajili ya kujitambulisha kwa usalama zaidi.
Amesema mashirika haya ni yale yenye miradi inayoanzia Shilingi milioni 20 na kuendelea na yaliyo chini ya hapo pia.

Amesesisitiza mashirika kutoa taarifa za kila robo ya mwaka ili mkoa uweze kutambua uwepo wa shirika husika na kuweza kusimamia maendeleo yake kwa ujumla.
 
 “Naomba nitumie fursa hii kuyasihi mashirika yote yanayotekeleza shughuli zake ndani ya mkoa wa Shinyanga, wafike ofisi ya mkuu wa mkoa wajitambulishe hususani yake miradi yao inaanzia milioni 20 na kuendelea na lazima uwe na vibali elekezwa kutoa ofisi ya Rais Tamisemi” Amesema Gunje

Na kuongeza “Lakini wale ambao miradi yao ni ya chini wafike ofisini kabla ya kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa ajili ya usalama wao, na kwa ajili ya kutekeleza miongozo na usimamizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ndani ya mkoa wetu” 

ELIMU KUTOKA NSSF

Elimu kutoka mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) mkoa wa Ki-NSSF Kahama iliyotolewa na Margareth Mwaibasa (Senior Compliance officer), amewataka wajasiriamali kuchangamkia fursa ya uwepo wa mfuko maalum wa ‘Hifadhi Skimu’ inayomwezesha kila mwananchi/mjasiriamali kujiwekea akiba ili kuongeza wigo wa Hifadhi ya jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma zinazotolewa na NSSF ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wan chi.


Amesema Skimu hiyo pia itasaidia juhudi za serikali za kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi wake, kuongeza nguvu za uzalishaji mali na kukuza uchumi wan chi pamoja na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.


Skimu hii imewalenga wajasiriamali na wananchi waliojiajiri wakiwemo Bodaboda, machinga, wachimbji wadogo wa madini, wakulima, wafugaji, mama/baba lishe, sanaa mbalimbali, wavuvi na biashara nyingine ndogondogo.


Amesema kila mwananchi mwenye umri wa miaka 15 hadi 70 anaruhusiwa kujiandikisha kwenye Hifadhi Skimu, inatayomwezesha kupata mafao ya pensheni ya uzee, mafao ya urithi, mafao ya ulemavu, uzazi, matibabu,na mafao ya kujitoa kwa maana ya kuchukua sehemu ya michango au michango yote pamoja na mafao ya msaada wa mazishi.


“Kundi hili na lenyewe linapaswa kuweka akiba zao za uzeeni, kwa sababu anaanza kufanya shughuli zake akiwa kijana lakini naye uzee pia utamkuta, na hili nikundi kubwa sana ambalo halikuwa na mahali pa kuweka akiba zake za uzeeni hata kama anatamani, sasa NSSF imekuletea Hifadhi Skimu kila mtu anufaike na mafao mbalimbali na yenye faida na faraja yanayopatikana hapa” Amesema 


Pamoja na hilo amewakumbusha waajiri kuhakikisha wanapeleka kwa wakati michango ya wanachama wao kama sheria inavyoelekeza kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na mwajiri kuchukuliwa hatua za kisheria.

ELIMU KUTOKA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA (TRA)

Akitoa elimu kuhusu maswala ya kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, Afisa usimamizi wa kodi kutoka mkoa wa kikodi Kahama Khamis Sanze amewakumbusha wamiliki wa mashirika kuzingatia utaratibu wa uanzishwaji wa mashirika hayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanasajiliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Amesema ni takwa la kisheria kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia mashirika yasiyo ya kiserikali, na kwamba endapo shirika husika halifanyi biashara basi litatakiwa kufuata utaratibu wa kuwasilisha maombi ya msamaha wa kodi kwa kamishna ya kodi.

Ni takwa la kisheria kwamba tunatakiwa tufanye kazi kwa kuzingatia STK (Sheria, Taratibu na kanuni), kwa hiyo unapoanzisha NGO, vitu vya msingi vya kuzingatia ni lazima ufanye kwanza usajili, na kwetu “TRA ili tukusajili cha kwanza lazima uwe na katiba au muhtasari wa kikao, cheti kutoka kwenye mamlaka inayohusika na usajili wako, nakala ya kitambulisho (NIDA, Leseni ya udereva au hati ya kusafiria, mkataba wa pango kama eneo utakuwa umepangisha na kama eneo ni la kwako utatuletea hati ya nyumba pamoja na barua ya utambulisho kutoka kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa ambapo biashara/asasi yako ipo“ Sanze

ELIMU KUTOKA TAKUKURU
Naye Happiness Bilakwate Afisa muelimishaji kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa wilaya ya Kahama ameyasihi mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia suala la uadilifi/maadili ikiwa ni pamoja na kufuata miongozo ya usajili wao na kuepuka viashiria vyote vya rushwa.

Ametaja mambo kadhaa yanayosababisha kuvunja maadili kuwa ni Pamoja na kutozingatia malengo ya uanzishaji ya NGO, mashirika mengi hayaajiri wataalamu kwenye maeneo ya msingi , uwiano wa huduma kwa Watoto kwenye vituo vilivyoanzisha kwa shughuli hiyo haupo sawa, kutowathamini watoa huduma wanaowaajiri

“Kwenye hizi NGO’s unakuta wengi wakizifungua wanasahau malengo yao ya uanzishaji wa shirika, kwa hiyo badala ya kujikita kwenye malengo wanakuwa wanafanya biashara jambo ambalo ni kinyume na maadili, kwa sababu unakuwa umedanganya” Amesema Happyness

Amesema yapo mashirika yanayokiuka mila na desturi za Mtanzania kwa kujihusisha katika mambo yasiyofaa na yaliyo kinyume na usajili wao ikiwemo Rushwa pamoja na kutumika kisiasa na baadhi ya wanasiasa wasiokuwa na nia njema na Taifa, badala yake kutaka kujinufaisha wao wenyewe. 
Senior compliance Officer

MWISHO.
 Senior compliance Officer kutoka NSSF Margareth Mwaibasa
 Happiness Bilakwate Afisa muelimishaji kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa wilaya ya Kahama


Afisa Maendeleo ya jamii wa Mkoa wa Shinyanga Bestina Gunja, akizungumza.














Post a Comment

Previous Post Next Post