Kijana mwenye maono mapana na ari ya kuwatumikia wananchi, Kasimu Saidi Mzee Matimbwa, leo amejitokeza rasmi kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea Ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, mkoani Morogoro.
Akiwa na umri wa miaka 33 tu, Kasimu Matimbwa anatajwa kuwa mmoja wa wagombea vijana kabisa kuwahi kuonesha nia ya kugombea nafasi hiyo ndani ya Jimbo hilo. Alichukua fomu hiyo mapema leo katika Ofisi za CCM Wilaya ya Morogoro Vijijini.
Kasimu Matimbwa ni mtaalamu wa Maji na Miamba (Hydrogeologist), mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka tisa katika sekta hiyo, akiwa miongoni mwa Wataalam wachache waliobobea fani hiyo nchini. Kasimu Matimbwa amesema anaamini kuwa maarifa yake ya kitaalamu na uzoefu wake wa miaka mingi katika kuleta huduma za maji safi na salama kwa wananchi, vinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Morogoro Kusini.
"Nimejifunza mengi kwa miaka yote hii nikiwa kwenye miradi ya maji nchini kote, sasa ni muda wa maarifa hayo kuletwa kwa wananchi wa Morogoro Kusini kupitia uwakilishi imara. Mimi si mgombea wa maneno, mimi ni mgombea wa Vitendo. Ninaweza, na nafaa."
Kasimu ameongeza kuwa anaingia katika kinyang'anyiro hicho akiwa na maono mapana ya kuleta mabadiliko makubwa, hasa kwa vijana na wakulima, ambao amesema wamekuwa wakikosa fursa za kujiendeleza kutokana na ukosefu wa huduma za msingi kama vile maji na miundombinu bora, ikiwemo barabara.
"Sisi vijana hatupaswi kusubiri nafasi tutafutiwe – ni wakati wetu kuamka, kuonesha uwezo wetu kumsaidia Mh. Rais katika Nchi. Nimeamua kusimama kwa ajili ya Morogoro Kusini, kwa sababu naamini naweza kuleta mabadiliko chanya. Niko tayari na nina kila sababu ya kuamini kuwa wananchi watanipa ridhaa hii."
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Morogoro Kusini wameonyesha matumaini makubwa kwa Kasimu, wakimtaja kama "kiongozi kijana, mwenye upeo, asiye na historia ya ubinafsi, na anayeelewa changamoto za wananchi."
Hii ni ishara kuwa mchakato wa uchukuaji fomu za kuwania ubunge kupitia CCM unaendelea kwa kasi mkoani Morogoro, huku majina mapya na yenye mvuto yakijitokeza kila uchao, likiwemo jina la Kasimu Saidi Mzee Matimbwa, ambalo sasa linatajwa kama chaguo jipya la matumaini kwa wakazi wa Morogoro Kusini.
MWISHO.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment