" MAAFISA USTAWI WA JAMII KAGERA WAAGIZWA KUTOA USHIRIKIANO KWA MASHIRIKA

MAAFISA USTAWI WA JAMII KAGERA WAAGIZWA KUTOA USHIRIKIANO KWA MASHIRIKA


Na Lydia Lugakila, Misalaba Media -Bukoba

Serikali mkoani Kagera imewataka maafisa ustawi wa jamii katika Halmashauri zote za Mkoa kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa karibu na mashirika mbalimbali, ikiwemo shirika la Tekla, ili kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu.

Kauli hii imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Hamis Maiga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajat Fatma Mwassa, katika hafla ya ugawaji vifaa na nyenzo za msaada kwa watoto wenye ulemavu kutoka shule sita za Mkoa wa Kagera. 

Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Gyamkana Manispaa ya Bukoba, kuelekea siku ya mtoto wa Afrika inayofanyika kila mwaka Juni 16.

Kanali Maiga amesisitiza kuwa serikali, chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, inajitahidi kuwahudumia watoto wenye ulemavu kwa kuwajengea shule maalum katika kila Halmashauri, pamoja na kuweka miundombinu rafiki ili watoto hao wapate haki zao za msingi.

 Ameagiza maafisa ustawi wa jamii kuongeza juhudi zao ili kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu.

"Naagiza maafisa ustawi wa jamii kutoa ushirikiano kwa mashirika kama Tekla, kwani wapo watoto wanaohitaji elimu pamoja na mahitaji mengine hivyo juhudi za pamoja zinahitajika ili kupunguza changamoto hizo" alisema Kanali Maiga.

Ameongeza kuwa serikali imejenga mabweni bora, kuwapatia watoto chakula bure na kuhakikisha wana lishe bora, huku akihimiza wadau mbali mbali kushiriki katika kutimiza ndoto za watoto hao bila ubaguzi.

"Watoto wetu wasijisikie wanyonge Mwenyezi Mungu ametuweka ili tuwasaidie kutimiza ndoto zao mimi nawashukuru sana Tekla kwa hafla hii kubwa," alisisitiza DC Maiga.

Shirika la Tekla Kagera, lililoanzishwa mwaka 2001 na kusajiliwa rasmi mwaka 2015, linajishughulisha katika masuala yanayohusiana na watu wenye ulemavu, hususan wanawake, watoto, na vijana. 

Mkurugenzi wa Tekla Kagera, Jackline Fabian, ameeleza kuwa hafla hiyo ilikuwa maalum kuelekea siku ya mtoto wa Afrika, wamewalwta pamoja watoto hao ikiwemo kupata chakula cha pamoja nao na  kuwakabidhi vifaa na maandalizi ya hafla vilivyogharimi jumla ya shilingi milioni 8 na laki 7 kwa watoto wenye ulemavu kutoka shule mbalimbali, akiwemo Msingi Tumaini, Lyamahoro (A), Rubale, Kagondo (B), na Mugeza viziwi.

Amesema vfaa vilivyotolewa ni pamoja na viti vyenye magurudumu, madaftari, pampas, kalamu, sare za shule, na viatu.

"Tekla inapongeza Serikali kwa juhudi za kuendeleza haki ya Elimu kwa watoto wenye ulemavu, na tunaona mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa elimu kwa wote," alisema Mkurugenzi huyo. 

Ameongeza kuwa katika kuwahudumia wanafunzi wenye ulemavu wamepata ushirikiano wa kutosha kutoka serikalini hasa Ofisi ya mkoa wa Kagera  na Halmashauri wanazofanya nazo kazi na wadau mbali mbali.

Aidha Bi Jackline amesema pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa walimu wa Elimu maalum, upungufu wa wadau wa kushirikiana na shirika hilo katika utoaji wa huduma kwa watoto, Wanawake na vijana wenye ulemavu.

Hata hivyo kwa upande wake Mwenyekiti wa shirika la Tekla Kagera Bi Analise Rubago amewaomba wadau mbali mbali kuendelea kuliunga mkono ili kuwanusuru watoto wenye uhitaji.

Hata hivyo ameipongeza Wilaya ya Missenyi kwa namna ilivyopiga hatua katika kufanya kazi kubwa kwa watu wenye ulemavu kwani mapato yao ya ndani wametenga fungu na kutoa vifaa saidizi, ikiwemo viti mwendo, fimbo nyeupe kwa watu wenye ulemavu ambapo suala hilo wamelipa kipaumbele.



Post a Comment

Previous Post Next Post