" MRADI WA TABLET KWA SHULE ZA MSINGI WATAMBULISHWA NGAZI YA MKOA WA SHINYANGA NA WILAYA

MRADI WA TABLET KWA SHULE ZA MSINGI WATAMBULISHWA NGAZI YA MKOA WA SHINYANGA NA WILAYA


Na. Paul Kasembo – Shinyanga RS.

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Imagine Worldwide Tanzania imetambulisha rasmi Mradi wa Msingi TEK, unaolenga kuboresha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa madarasa ya Kwanza, Pili na Tatu katika shule za msingi nchini.

Mradi huu wa majaribio utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika jumla ya shule 533 nchini. Kati ya hizo, shule 500 zinapatikana katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Morogoro, Ruvuma na Manyara, huku shule 33 zikiwa Zanzibar. Kwa Mkoa wa Shinyanga, utekelezaji umeanza katika Wilaya za Shinyanga na Kishapu, ambapo shule 100 zinanufaika moja kwa moja.

Akizungumza katika kikao kazi na uongozi wa Mkoa wa Shinyanga, Mkurugenzi wa Shirika la Imagine Worldwide Tanzania, Dkt. Jacqline Mgumia, alieleza kuwa mradi huu ni matokeo ya ushirikiano kati ya shirika lake na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Kupitia mradi huu, shule shiriki zitapatiwa vishkwambi (tablets) vyenye programu maalum ya lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kujifunza stadi za msingi kwa njia ya video za elimu, michezo ya kujifunzia na hadithi, katika mazingira yanayowahusisha moja kwa moja. Ili kuwezesha matumizi endelevu ya vifaa hivyo, shule husika zitafungiwa miundombinu ya umeme wa jua kwa ajili ya kuchaji vifaa, pamoja na kuunganishwa na intaneti, itakayowezesha ufuatiliaji wa matumizi na tathmini ya maendeleo ya wanafunzi.

Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP. Salum Hamduni, Bw. David Lyamongi alishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu kupitia miradi ya kimkakati kama huu. Vilevile, aliipongeza Imagine Worldwide kwa ushirikiano wao na Serikali, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza vifaa vya mradi ili viweze kutumika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Camara Education Tanzania, ambao ni watekelezaji wa mradi kwa Mkoa wa Shinyanga, alieleza kuwa kuanzia wiki hii, wataanza kutembelea shule 10 za awali kwa ajili ya kufanya tathmini za mazingira, kabla ya kuanza ufungaji wa vifaa ifikapo mwanzoni mwa mwezi Julai. Aidha, walimu katika shule hizo watapatiwa mafunzo maalum ya matumizi ya vishkwambi na mbinu bora za kufundisha kwa kutumia teknolojia.

Naye Mkurugenzi wa Programu wa Imagine Worldwide, Bi. Jenny Lindgren, alifafanua kuwa mradi huu pia unatekelezwa katika nchi za Malawi, Senegal na Sierra Leone, na umekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha stadi za KKK, kuongeza mahudhurio ya wanafunzi darasani, pamoja na kupunguza changamoto mbalimbali kama vile upungufu wa walimu, vifaa vya kujifunzia na uhaba wa vitabu.

Mradi wa Msingi TEK unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu ya msingi nchini, na matokeo ya awali ya majaribio haya yatachochea upanuzi wa mradi kitaifa, kama sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha elimu jumuishi, jumuishi na jumuishi kwa wote.



























 


















Post a Comment

Previous Post Next Post