" NAIBU MEYA ZAMDA: ATOA WITO WA KUTUNZA MAZINGIRA KWA USTAWI WA VIZAZI VIJAVYO, EZRA MANJERENGA: ASISITIZA UDHIBITI WA PLASTIKI KUELEKEA MAZINGIRA ENDELEVU

NAIBU MEYA ZAMDA: ATOA WITO WA KUTUNZA MAZINGIRA KWA USTAWI WA VIZAZI VIJAVYO, EZRA MANJERENGA: ASISITIZA UDHIBITI WA PLASTIKI KUELEKEA MAZINGIRA ENDELEVU

Na Mapuli Kitina Misalaba

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Zamda Shaban Mwebea, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda na kutunza mazingira, akisisitiza kuwa suala hilo ni jukumu la kila mmoja kwa ustawi wa jamii ya sasa na vizazi vijavyo.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika leo Juni 5, 2025 katika maeneo mbalimbali Manispaa ya Shinyanga ambayo yameambatana na zoezi la kufanya usafi katika maeneo ya soko la Ngozonane, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utamaduni wa usafi na uhifadhi wa mazingira kwa vitendo.
“Jambo la mazingira ni letu sote, kila mmoja anahusika. Tunatakiwa tuhifadhi mazingira yetu ili na sisi yaweze kutuhifadhi, tutunze mazingira yetu ili na sisi yaweze kututunza, ikiwa ni pamoja na kupanda miti, tusikate miti ovyo.”amesema Zamda.

Ameongeza kuwa kufanya usafi mara kwa mara si tu kunalinda mazingira bali pia kunachangia katika afya bora za wananchi:
“Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mazingira safi na maisha bora ya mwanadamu. Wazazi wetu walitupandia miti na kutuachia mazingira rafiki; nasi tuendelee kupanda miti ili na vizazi vyetu vipate mazingira bora ya kuishi.”amesema Zamda

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mazingira na Maliasili wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga, amesema serikali inasisitiza wananchi kuwajibika katika kutunza mazingira sambamba na kudhibiti matumizi ya plastiki.

Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba ujumbe mzito wa kuhimiza jamii kuchukua hatua sasa.

“Ujumbe wetu mwaka huu unatusisitiza cha kwanza tuwe na wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira ili tuwe na haki ya kuyatumia mazingira yetu. Lakini la pili ni matumizi na udhibiti wa plastiki, kwa hiyo ujumbe wetu pia ni kuhakikisha tunakuwa na matumizi salama na endelevu ya plastiki,” amesema Manjerenga.

Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni:
“Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa; Dhibiti Matumizi ya Plastiki,” ambayo inalenga kuelimisha umma kuhusu madhara ya taka zisizooza na kuhimiza matumizi ya mifuko mbadala.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga waliohudhuria maadhimisho hayo wameeleza kufurahishwa na ushiriki wao katika shughuli za utunzaji wa mazingira, wakisisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anahifadhi mazingira kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Wamesema utunzaji wa mazingira unasaidia kuzuia magonjwa, kuboresha mandhari ya maeneo ya makazi na kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Maadhimisho haya ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga katika kuhimiza ushiriki wa jamii kwa vitendo katika kukabiliana na changamoto za kimazingira ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Zamda Shaban Mwebea, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Zamda Shaban Mwebea, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Zamda Shaban Mwebea, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.Mkuu wa Idara ya Mazingira na Maliasili wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.Mkuu wa Idara ya Mazingira na Maliasili wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.Zoezi la usafi wa Mazingira likiendelea.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Zamda Shaban Mwebea, akiongoza maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika leo Juni 5, 2025 mjini Shinyanga.













 

Post a Comment

Previous Post Next Post