" RAIS DKT. SAMIA : HALI YA UCHUMI WA TAIFA IMEZIDI KUIMARIKA

RAIS DKT. SAMIA : HALI YA UCHUMI WA TAIFA IMEZIDI KUIMARIKA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia na kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 June, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma tarehe 27 June, 2025.

…………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa hali ya uchumi wa nchi imeendelea kuimarika, ambapo kwa mwaka 2025 kasi ya ukuaji wa uchumi inakadiriwa kufikia asilimia sita.

Aidha, pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021 hadi kufikia trilioni 205.84 mwaka 2024, sambamba na kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.

Akizungumza leo, Juni 27, 2025, jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia amesema kuwa kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania mwaka 2025 inatarajiwa kufikia asilimia 6.

Dkt. Samia ameeleza kuwa kiashiria kingine cha utulivu wa uchumi ni mfumuko wa bei, ambao umeendelea kubaki chini ya asilimia 5 kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, hali inayoendana na malengo ya taifa ya kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki chini ya kiwango hicho.

“Mfumuko wa bei tulionao ni miongoni mwa viwango bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na upo chini ya wastani wa mfumuko wa bei Barani Afrika. Hali hii inachangiwa na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, pamoja na uhakika wa upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani,” amesema Rais Dkt. Samia.

Kuhusu biashara ya kimataifa, Rais Samia amesema kuwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 6.39 mwaka 2021 hadi kufikia dola bilioni 8.7 mwaka 2024, jambo lililosaidia kuimarisha akiba ya fedha za kigeni.

Aidha, ameeleza kuwa kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweza kununua na kuhifadhi akiba ya dhahabu yenye thamani ya trilioni 3.424, ambapo hadi sasa tayari dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 702.3 imenunuliwa na ununuzi unaendelea.

Kuhusu masuala ya kodi, Dkt. Samia alisisitiza kuwa anapendelea kuona wafanyabiashara na wawekezaji wanaelimishwa kuhusu umuhimu wa kodi badala ya kutumia nguvu katika ukusanyaji wake.

Amesema kuwa kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kuwatia moyo walipaji wa kodi.

“Serikali imeimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato, kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, kuanzisha jukwaa la kodi kwa wawekezaji, na kuongeza uwezo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” amefafanua.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zimechangia kuongeza mapato ya ndani kwa mwezi kutoka shilingi trilioni 1.51 mwezi Novemba 2020 hadi kufikia trilioni 3.09 mwezi Machi 2025.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post