" UMOJA WA WANAUME TANZANIA WAKUTANA NA KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII

UMOJA WA WANAUME TANZANIA WAKUTANA NA KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII

Na Mapuli Kitina Misalaba 

Viongozi wa Umoja wa Wanaume Tanzania (Wanaume Wanaojitambua) wamefanya kikao muhimu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. John Jingu, kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma, kwa lengo la kuutambulisha rasmi Umoja huo kwa Serikali na kujadili mikakati ya ushirikiano kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Umoja huo, Ndg. Claude Benedict Kimu, alieleza kwa kina historia ya kuanzishwa kwa Umoja wa Wanaume Tanzania, malengo yake na mpango mkakati wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazolenga ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu na viongozi waandamizi wa Wizara, Ndg. Kimu alibainisha kuwa Umoja huo ulianzishwa kwa dhamira ya kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii kupitia programu zinazowalenga wanaume, hususan katika masuala ya malezi bora ya watoto, maadili, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, na uwezeshaji kiuchumi kwa wanaume.

Katika hatua nyingine ya kikao hicho, Mhe. Dkt. Jingu alimkabidhi rasmi Mwenyekiti huyo miongozo mbalimbali ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji, ikiwa ni pamoja na maboresho ya Sera ya Wazee, masuala ya maadili, na sera za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii.

Kwa upande wake, Ndg. Kimu alimkabidhi Katibu Mkuu nyaraka muhimu za Umoja huo ikiwemo Katiba ya Umoja, Cheti cha Usajili, Masharti ya Usajili na Cheti cha Utambulisho wa Mlipa Kodi, kama uthibitisho wa uhalali wa taasisi hiyo kijamii na kisheria.

Wakati wa kufunga kikao, Mhe. Dkt. Jingu aliwapongeza viongozi wa Umoja wa Wanaume Tanzania kwa ujasiri na uzalendo waliouonesha kwa kuanzisha taasisi hiyo kwa kutumia rasilimali zao binafsi bila msaada kutoka nje. Alisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara yake ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Umoja huo katika utekelezaji wa malengo yake ya kijamii.

"Kwa kweli mnastahili pongezi. Kwa muda mfupi wa takribani miezi minane tangu mmesajiliwa, mmeonyesha dhamira ya kweli ya kubadilisha jamii. Serikali iko pamoja nanyi," alisema Mhe. Dkt. Jingu.

Ameeleza kuwa Serikali inaupokea Umoja huo kama mshirika muhimu katika kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii kama vile ukatili wa kijinsia, mmomonyoko wa maadili, watoto wa mitaani, usagaji, ushoga, ulawiti, matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na kuhakikisha watoto wa kiume hawasahauliki katika agenda ya malezi bora.

Kwa kauli moja, kikao hicho kimefunguliwa kwa matumaini makubwa ya ushirikiano kati ya Wizara na Umoja wa Wanaume Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya jamii.


Kauli Mbiu:

"WANAUME – NGUZO YA JAMII"













🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post