Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Uwezo wa kisiasa na ushawishi wa Mhandisi James Jumbe
unaendelea kuvutia hata nje ya mipaka ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya
Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA kupitia ACT Wazalendo,
Emmanuel Ntobi, kuonesha wazi kutamani kushirikiana naye katika harakati za
kuwatumikia wananchi.
Kupitia ujumbe wake wa
hadharani, Ntobi amemwelezea Jumbe kama kiongozi mwenye mvuto na anayekubalika
kwa wananchi wa Shinyanga Mjini, akisisitiza kuwa taifa linahitaji viongozi wa
aina hiyo wenye maono na ushawishi wa kweli.
Si kawaida kwa chama cha
upinzani kumvutiwa waziwazi na mwanasiasa kutoka chama tawala, lakini mchango
na mwenendo wa Jumbe umeonesha tofauti kubwa na kuwafanya wapinzani waone
umuhimu wa kuungana naye katika mustakabali wa kisiasa wa taifa.
“Tunamkaribisha
ACT – chama cha vitendo – tukapambane kwa ajili ya wananchi. Safari hii,
tunahitaji ushindani wa haki bila kubughudhiwa na vyombo vya dola. Wananchi
wanahitaji mtu jasiri, si maneno matupu!”amesema Ntobi
Kauli hiyo inakuja muda mfupi baada ya Jumbe kutoa
salamu za shukrani kwa CCM na kueleza kuwa licha ya kutopitishwa kuwania
ubunge, ameendelea kujifunza mengi, na yupo tayari kuendelea kulitumikia taifa
kwa namna yoyote ile itakayowezekana.
Kwa wachambuzi wa siasa mkoani Shinyanga, kauli ya ACT Wazalendo imechukuliwa kama ishara ya wazi kuwa Jumbe ni kiongozi mwenye mvuto mpana unaovuka mipaka ya chama kimoja, huku wananchi wakisubiri kwa hamu kuona hatua yake inayofuata.
Post a Comment