
Mwenyekiti wa Kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng’ombe, Juma Bugohe, akizungumza kwenye kikao cha pamoja.Na Mapuli Kitina Misalaba
Wanakikundi wa Shinyanga Chapa ya Ng’ombe, waliopo Kata ya Old Shinyanga, wamekubaliana kwa pamoja kuanza kushirikiana kwa karibu zaidi katika nyakati za shida na raha, ikiwemo misiba, sherehe, ajali, magonjwa na maafa mbalimbali yanayoweza kuzikumba familia zao, kwa lengo la kurahisisha utatuzi wa changamoto pindi zinapojitokeza.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha pamoja cha wanachama wa kikundi hicho, ambacho pia kilikwenda sambamba na kupitishwa kwa rasimu ya katiba ya kikundi.
Katika kikao hicho, viongozi wa kikundi wamepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wanachama na kuyajadili kwa kina, kabla ya kukubaliana kwa pamoja misingi ya uendeshaji wa kikundi hicho.
Kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng’ombe kina jumla ya wanachama 83, ambapo wanachama waliohudhuria kikao hicho walionesha furaha na kuridhishwa na maamuzi yaliyofikiwa, wakieleza kuwa ushirikiano huo utaimarisha mshikamano, kurahisisha maandalizi ya sherehe mbalimbali, na kuwa nguzo muhimu ya kusaidiana wakati wa changamoto nzito kama magonjwa yanayohitaji matibabu ya muda mrefu pamoja na ajali zitakazotokea.
Baadhi ya walezi wa kikundi hicho, akiwemo Enock Lyeta na Pika Chogelo, wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu na uwajibikaji wa kila mwanachama ambapo wamewahimiza wanachama kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kutoa ada na michango waliyokubaliana, iwe ni wakati wa shida au raha, ili kufanikisha malengo ya kikundi.
Aidha, walezi hao wameonya dhidi ya kuwaruhusu watu wenye nia mbaya kujiunga au kuvuruga amani ya kikundi, ikiwemo kuingiza masuala ya kisiasa huku wakieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha mshikamano na hata kusababisha kuvunjika kwa kikundi, jambo ambalo halikubaliki.
Katika kikao hicho, mmoja wa walezi wa kikundi ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Wilaya ya Shinyanga, Hasna Maige, ametumia fursa hiyo kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili.
Amewasisitiza wanachama kuendelea kuwa mabalozi wa amani na kuepuka vitendo vyote vya ukatili, ikiwemo unyanyasaji na kunyimana haki ndani ya kikundi.
Hasna Maige amewahimiza pia wanakikundi kukemea vitendo vya ukatili vinavyojitokeza katika jamii, na kutoa taarifa kwa viongozi husika pindi vitendo hivyo vinapotokea.
Ameeleza kuwa taarifa zinaweza kutolewa kwa viongozi wa kikundi, serikali za mitaa, viongozi wa dini, viongozi wa SMAUJATA au kupitia namba ya bure 116, ili serikali iweze kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng’ombe, Juma Bugohe, amesema kikundi hicho kimeanzishwa kutokana na uzoefu wa jamii ya eneo hilo kukumbwa na majanga mbalimbali bila kupata msaada wa haraka, hali iliyosababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza ndugu kwa kukosa fedha za matibabu.
Amesema kikundi hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake, hasa katika kukabiliana na changamoto zinazowakumba familia zao ikiwemo ukosefu wa fedha za matibabu, ajali, na maafa mengine ya kijamii.
Juma Bugohe amewahimiza wanachama kuendelea kushirikiana, kupendana na kuzingatia taratibu na miongozo waliyojiwekea ili kufikia malengo ya kikundi.
Pia amesisitiza kuwa kikundi hicho hakina mwelekeo wa kisiasa wala hakitajihusisha na masuala ya siasa, bali litaendelea kutekeleza lengo lake kuu la kusaidiana kijamii.
“Tumekuwa tukikumbwa na majanga mbalimbali bila msaada wa kutosha, lakini kupitia rasimu ya katiba yetu, kikundi hiki kitatusaidia sana. Si kikundi cha kisiasa, hivyo tuendelee kuheshimiana, kupendana na kusaidiana. Pale tatizo linapotokea liwe la kweli, kwani tukibaini udanganyifu tutachukua hatua kali ikiwemo kumfuta mwanachama,” amesema Bugohe.
Kwa ujumla, wanachama wa Shinyanga Chapa ya Ng’ombe wameonesha dhamira ya dhati ya kujenga mshikamano wa kijamii, kusaidiana kwa vitendo, na kuimarisha ustawi wa familia zao kupitia umoja na uwajibikaji wa pamoja.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng’ombe, Juma Bugohe, akizungumza kwenye kikao cha pamoja.
Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Wilaya ya Shinyanga, Hasna Maige, akitoa elimu ya masuala ya ukatili kwenye kikao hicho.
Mmoja wa walezi wa kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng'ombe, Mchungaji Enock Charles Lyeta akizungumza kwenye kikao hicho.
Mmoja wa walezi wa kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng'ombe, Pika Chogelo akizungumza kwenye kikao hicho cha pamoja.
Wanachama wa kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng'ombe wakiwa katika kikao cha pamoja.
Wanachama wa kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng'ombe wakiwa katika kikao cha pamoja.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254









































Post a Comment