Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera Uongozi wa Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Hajjat Fatuma Mwassa, umepongezwa kwa kubuni Tamasha la Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani) ambalo limefanikiwa kuwahamasisha wana Kagera wanaoishi nje ya mkoa huo, ndani na nje ya nchi, kurejea nyumbani na kushiriki kikamilifu katika kuendeleza uchumi na utamaduni wa mkoa.Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene, alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Tamasha la Utamaduni lililofanyika Desemba 21, 2025, ikiwa ni sehemu ya Tamasha kubwa la Ijuka Omuka. Waziri Simbachawene alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi.Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Simbachawene amesema kuanzishwa kwa Tamasha la Ijuka Omuka kumeibuka kuwa chachu kubwa ya kuwakutanisha wana Kagera na kuhamasisha uwekezaji wa maendeleo katika mkoa wao wa asili, hatua ambayo imeanza kuurejesha mkoa huo katika ubora wake wa kiuchumi na kijamii. “Nimekutana na marafiki zangu wengi hapa ambao sikujua kama ni wazaliwa wa Mkoa wa Kagera. Kwa kweli wazo hili ni jema na limeleta matokeo chanya kama nilivyoelezwa. Si vibaya mikoa mingine ikaiga mfano huu. Mimi nitaanza kumsahauri Mkuu wa Mkoa wangu wa Dodoma, Mhe. Rose Senyamule, nasi tufanye. Nimeona mambo mengi mazuri na ni dhahiri kuwa utamaduni wa Mkoa wa Kagera umetunzwa vizuri,” amesema Mhe. Simbachawene.Aidha, Waziri huyo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuendelea kutumia vyema fursa ya mvua zinazonyesha mara mbili kwa mwaka kwa kuongeza uzalishaji wa mazao, hususan kahawa, akibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bei ya zao hilo imeongezeka kwa kiasi kikubwa. “Uzalishaji wa kahawa umeupatia mkoa huu shilingi bilioni 232 ambazo zimelipwa moja kwa moja kwa wakulima, pamoja na ushuru wa halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 7.3 kwa msimu wa mwaka 2025/2026,” ameongeza.Awali akitoa salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatuma Mwassa, amesisitiza utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano unaolenga kutengeneza nafasi za ajira zipatazo 16,000 kupitia miradi midogo midogo ya vijana katika sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda vidogo, pamoja na kuimarisha na kuanzisha kongani mpya. “Mkakati huu utafanikiwa kwa vitendo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo SIDO, VETA na wadau wengine wa maendeleo,” amesema Mkuu wa Mkoa.Katika hatua nyingine, akizungumza kuhusu historia ya kupanda na kushuka kwa Ngome ya Buhaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Bonaventura Ishengoma Rutinwa, amesema kuwa shughuli za kilimo hususan uzalishaji wa ndizi na kahawa pamoja na ufugaji wa Ng’ombe ndizo zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera miaka ya nyuma.Tamasha la Utamaduni, lililojumuisha maonesho ya bidhaa na urithi wa kiutamaduni wa Kagera, ni sehemu ya Tamasha la Ijuka Omuka lililozinduliwa Desemba 18, 2025 na kufikia kilele chake Desemba 21, 2025 mkoani Kagera.🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254





Post a Comment