" WAHITIMU 353 WANG’ARA MAHAFALI YA KWANZA YA CHUO CHA SERIKALI ZA MITAA KAMPASI YA SHINYANGA

WAHITIMU 353 WANG’ARA MAHAFALI YA KWANZA YA CHUO CHA SERIKALI ZA MITAA KAMPASI YA SHINYANGA

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif akizungumza katika mahafali ya kwanza Chuo cha Serikali za Mitaa Kampasi ya Shinyanga.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumla ya wanachuo 353 wamehitimu mafunzo yao katika Mahafali ya kwanza ya Chuo cha Serikali za Mitaa Kampasi ya Shinyanga yaliyofanyika leo Desemba 19, 2025.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Dk. Jafar Rajabu Seif, amesema chuo hicho kina mchango mkubwa katika kuzijengea uwezo mamlaka za serikali za mitaa kupitia utoaji wa mafunzo, tafiti na ushauri wa kitaaluma unaolenga kuimarisha utawala bora na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Serikali inatambua mchango wa chuo hiki katika kuzijengea uwezo mamlaka za serikali za mitaa kupitia mafunzo, tafiti na ushauri wa kitaaluma katika masuala ya mamlaka za serikali za mitaa,” amesema Mhe. Dk. Seif.

Dk. Seif, amekipongeza chuo kwa kuanzisha Kampasi ya Shinyanga ambayo kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake tayari imeanza kuzalisha wahitimu, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio makubwa katika kukuza rasilimali watu kwa ajili ya serikali za mitaa.

“Napenda kuwapongeza kwa dhati kwa kuanzisha tawi la Shinyanga ambalo leo tunashuhudia wahitimu wake. Kwa ujumla, serikali inaridhishwa na utendaji wa chuo kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi,” ameongeza.

Katika hotuba yake kwa wahitimu, Naibu Waziri amewasisitiza kuwa waadilifu, wazalendo na wachapakazi, wakitumia kikamilifu utaalamu na weledi walioupata wakati wa mafunzo yao chuoni, huku akibainisha kuwa wahitimu wa chuo hicho wana nafasi kubwa ya kunufaika na ajira zinazotolewa na mamlaka za serikali za mitaa pindi wanapokidhi vigezo vinavyohitajika.

Mahafali hayo yamehusisha wahitimu wa ngazi za Astashahada ya awali na Astashahada ya kwanza katika fani za Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha katika Serikali za Mitaa, Menejimenti ya Rasilimali Watu pamoja na Maendeleo ya Jamii.

Akisoma taarifa ya chuo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Kampasi ya Shinyanga, Dkt. Mashala Yusuph, amesema kampasi hiyo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 615 wanaosoma katika fani mbalimbali, huku ikiendelea kupanua wigo wa mafunzo kwa kutoa kozi kuanzia ngazi ya nne hadi ya sita.

“Chuo kinatoa kozi za Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha katika Serikali za Mitaa, Menejimenti ya Rasilimali Watu pamoja na Maendeleo ya Jamii kuanzia ngazi ya nne mpaka ya sita,” amesema Dkt. Yusuph.

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa kampasi hiyo kumewezeshwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa serikali imeendelea kukithamini chuo hicho kwa kukiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa weledi, ikiwemo kutoa fursa za ajira na mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, uongozi wa chuo umemshukuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga na sasa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Johari Samizi, kwa mchango wake mkubwa katika kuanzishwa kwa chuo hicho, akitambuliwa kama mmoja wa waanzilishi muhimu wa Kampasi ya Shinyanga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Mazindi, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, amewataka wahitimu kuwa watu wa vitendo na kujituma katika kazi na maisha yao ya kila siku.

“Kila mmoja aanze kuwaza anaifanyia nini Tanzania na anaifanyia nini Shinyanga. Fanyeni kazi kwa bidii muda wote, msije mkajidhalilisha taaluma zenu kwa kukaa mitaani au kujihusisha na michezo ya kubahatisha,” amesema DC Masindi.

Baadhi ya wahitimu waliozungumza baada ya mahafali hayo wamesema wapo tayari kuitumikia jamii kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni, huku wakiahidi kuendelea kuzingatia maelekezo ya serikali na kudumisha uzalendo wa taifa.

Wameishukuru serikali kwa kufungua Kampasi ya Chuo cha Serikali za Mitaa mkoani Shinyanga, jambo lililowaondolea gharama na usumbufu wa kufuata elimu mkoani Dodoma, na hivyo kuwapa fursa ya kusoma karibu na maeneo yao.

Mahafali hayo yamehitimishwa kwa zoezi la kuwatunuku wahitimu vyeti, tukio lililoashiria mwanzo mpya wa safari ya kitaaluma na utumishi kwa wahitimu wa kwanza wa Kampasi ya Shinyanga.

Aidha mahafali hayo yamehudhuriwa na viongozi wa serikali, wasimamizi wa elimu, wazazi na wanajamii kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dk. Jafar Seif, akizungumza katika mahafali ya kwanza Chuo cha Serikali za Mitaa Kampasi ya Shinyanga.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Kampasi ya Shinyanga, Dkt. Mashala Yusuph akisoma taarifa ya chuo hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Mazindi akizungumza kwenye mahafali hayo.

Viongozi wa serikali, uongozi wa chuo na wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mahafali leo Disemba 19, 2025.









Post a Comment

Previous Post Next Post