" ‎KYERWA: BARAZA LA WAFANYAKAZI LAFANYIKA, WATUMISHI WAHIMIZWA KUIMARISHA MAWASILIANO KAZINI

‎KYERWA: BARAZA LA WAFANYAKAZI LAFANYIKA, WATUMISHI WAHIMIZWA KUIMARISHA MAWASILIANO KAZINI

‎Na Fabius Clavery,  Misalaba Media -Kagera.

‎Watumishi wa Umma Wilaya ya Kyerwa wamehimizwa kuendelea kuimarisha ushirikiano, mawasiliano na kuzingatia taratibu za kiutumishi ili kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

‎Wito huo umetolewa  Disemba 17, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Mwl. Mayala Sengerema, wakati akiongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wilaya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.

‎Mwl. Sengerema amewaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa mabaraza ya wafanyakazi ni jukwaa muhimu linalowapa watumishi fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yatakayosaidia kutatua changamoto za kiutumishi na kuboresha ustawi kazini.

‎“Tuliopata fursa ya kuwa viongozi, tuna wajibu wa kusaidiana pale panapotokea changamoto za kiutumishi. Watumishi walioko ngazi za chini wanatutegemea sisi, hivyo ni muhimu kuhakikisha changamoto zao zinapata ufumbuzi kwa kuzingatia taratibu,”alisema Mwl. Sengerema.

‎Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TWALGWU) Mkoa wa Kagera, Ndg. Moses Bukuru, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kwa kuendelea kuketi Baraza la Wafanyakazi mara kwa mara, akisema hatua hiyo inachangia kuimarisha mahusiano kazini na kuongeza morali kwa watumishi.

‎Aidha, amepongeza utaratibu wa kuwatambua na kuwatuza wafanyakazi hodari kila mwaka, akibainisha kuwa huongeza motisha na kuwahamasisha watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi.

‎Baraza la Wafanyakazi wa Wilaya ya Kyerwa linajumuisha wajumbe kutoka Vyama vya Wafanyakazi vya TWALGWU, TUGHE na CWT, pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali, na hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.


Post a Comment

Previous Post Next Post