" Luhanga Mpina Apigwa Chini Mbio za Ubunge Simiyu

Luhanga Mpina Apigwa Chini Mbio za Ubunge Simiyu

 

Mbunge wa Jimbo la Kisesa anayemaliza muda wake Luhaga Mpina huenda safari yake ya kuwawakilisha wananchi wa Kisesa ikafikia tamati ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka huu baada ya vikao vya mchujo kwa ngazi ya wilaya ya Meatu na mkoa wake wa Simiyu kumtupa nje ya mbio za kuwania kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera kwenye nafasi ya ubunge katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu; vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya kikao cha kamati ya siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu.

Mpina Mbunge machachari ndani na nje ya Bunge aliyejipatia umaarufu kwenye takribani miaka mitano sasa kwa kuibana serikali ndani ya Bunge na hata nje ya Bunge kwa hoja mbalimbali amekumbana na rungu la chama chake ngazi ya wilaya na mkoa baada ya vikao vya Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Meatu kumtupa nje kwa kutopendekeza jina lake- maamuzi ambayo yamebarikiwa na chama ngazi ya mkoa hivyo sasa nafasi ya mwisho ya yeye kupenya jina lake kwa ajili ya kwenda kwenye mchakato wa kura za maoni ikibakia vikao vya ngazi ya taifa kwa maana ya Kamati Kuu ambayo imepewa mamlaka ya kufanya uteuzi wa mwisho.

Katika jimbo hilo, wagombea waliokuwa wakichuana katika hatua ya awali walifikia 14, lakini kupitia kikao cha wilaya na mkoa, majina yaliyopendekezwa ni Sitta Risinge, Mussa Mbuga, na Silinde Gumada.

Kiujumla, majina yote yaliyopendekezwa ngazi ya wilaya na mkoa hupelekwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa, na Kamati kuu hiyo ina uwezo wa kuja na mapendekezo yake ya majina kwa kurejea majina ya awali ya wote waliochukua fomu, waliopendekezwa nkwa upande wa wilaya na hata yale ya mkoa.

Baada ya hapo Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitapokea na kuchambua majina ya wagombea Ubunge kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya uteuzi, kisha Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitafikiria na kuteua majina ya WanaCCM wasiozidi watatu walioomba nafasi ya Ubunge na ili wakapigiwe kura za maoni na hatua zaidi ndani ya chama zitafuata kabla ya kumpata mgombea atakayekiwakilisha chama katika jimbo husika.

Post a Comment

Previous Post Next Post