Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Maxon Binomtonzi Barthazary, mkazi wa kijiji cha Nyabishenge, Kata ya Kaisho, wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, ameahidi makubwa kwa wana Kyerwa.
Maxon, ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Kyerwa, amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kuwa yuko tayari kushughulikia changamoto ya maji pamoja na kuleta maelewano ndani ya chama cha CCM endapo atapata ridhaa ya kuwa mwakilishi wa wananchi Bungeni.
Ametoa kauli hiyo akiwa katika mkutano na wanachama wa chama hicho uliofanyika kata ya Nkwenda, ambapo pia ameahidi kufanya kazi ya kuimarisha ushirikiano na kukuza maendeleo.
"Naombeni wana Kyerwa mniunge mkono katika safari yangu hii ya kuusaka ubunge Jimbo la Kyerwa," alisema mgombea ubunge huyo.
Amesema kuwa mwaka 2020 alijitokeza kuomba nafasi ya ubunge lakini kura hazikutosha, na pia mwaka 2022 alijaribu kuomba nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM taifa na pia hakuweza kufanikiwa.
Aidha, amesema kuwa bado ana nia ya dhati ya kuwatumikia wana Kyerwa, na anawaomba wamuamini.
Pia, amesisitiza kuwa amesoma na kupitia majukumu anayopaswa kuyatekeleza, na ameangalia ilani ya chama cha Mapinduzi kwa yale wanayotakiwa kuyatekeleza kwa wananchi, na yuko tayari kuwakilisha jimbo la Kyerwa.
Post a Comment