Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Mjumbe wa Kamati ya Siasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, ametoa shukrani zake kwa chama chake kwa kumpa nafasi ya kushiriki mchakato wa ndani wa kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo.
Kupitia ujumbe wake kwa wananchi wa Shinyanga Mjini, Mhandisi Jumbe amesema ameshiriki mchakato huo bila kukumbwa na changamoto yoyote na kwamba alikuwa tayari kuanzia hatua ya kuchukua fomu hadi hatua ya kurudisha, hali iliyomuwezesha kujifunza mengi kuhusu siasa na utaratibu mzima wa chama.
“Nashukuru chama changu CCM kwa kunipa fursa hii. Nimemaliza mchakato huu kwa amani na nimejifunza mengi katika hatua mbalimbali. Ingawa sijaingia kwenye hatua za juu zaidi, nimepokea maamuzi ya vikao kwa moyo mmoja,” amesema Jumbe.
Amesisitiza kuwa ataendelea kuwa mwanachama mtiifu na muaminifu wa CCM, na tayari ameanza kuipigia debe CCM kuhakikisha chama hicho kinaibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao. Ameahidi kushirikiana na wale wote waliopata nafasi ya kupeperusha bendera ya chama.
“Uongozi ni wa nyakati. Nitakuwa tayari wakati wowote chama changu kitakaponiona nafaa,” ameongeza Jumbe.
Amehitimisha kwa kusema kuwa ataendelea kuwa bega kwa bega na wananchi wa Shinyanga Mjini katika harakati mbalimbali za maendeleo huku akiwatakia kila la heri wagombea waliopita.
Post a Comment