" MJADALA WA MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO WAFANA RADIO FARAJA FM, SHINYANGA

MJADALA WA MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO WAFANA RADIO FARAJA FM, SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wamekutana leo Julai 9, 2025 katika ukumbi wa Redio Faraja FM kushiriki mjadala maalum kuhusu malezi na makuzi ya mtoto, ulioandaliwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na shirika la ICS Investing in Children and Strengthening their Societies (Creating Change).

Mjadala huo ambao pia umetangazwa mubashara kupitia Redio Faraja na kurasa zake za mitandao ya kijamii, umejumuisha washiriki kutoka Umoja wa Wanaume Mkoa wa Shinyanga, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali za mitaa, viongozi wa kimila, wataalamu wa ustawi wa jamii, watoto, wazazi na walezi pamoja na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali.

Katika mjadala huo, washiriki wamechangia maoni na uzoefu juu ya namna jamii inavyoweza kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yanayozingatia haki zao za msingi kama vile elimu, afya, ulinzi na fursa ya kuishi maisha ya furaha na usalama.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Lydia Kwesigabo, ameeleza kwa kina sheria na miongozo mbalimbali inayolinda haki na ustawi wa mtoto, akisisitiza kuwa malezi ya mtoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa familia, jamii na serikali.

Naye Afisa Mradi kutoka ICS, Bi. Lucy Maganga, amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uhamasishaji wa jamii juu ya malezi chanya, kwa kushirikiana na viongozi wa kimila, wa dini, pamoja na familia, ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye heshima kwa utu wao.

Akifunga mjadala huo, mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni mtangazaji wa Redio Faraja FM, Simeo Makoba, ameishukuru serikali ya mkoa kwa kuruhusu wataalamu wake kushiriki, na kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Mboni Mhita kwa ushirikiano.

Aidha, amelipongeza shirika la ICS kwa kushirikiana bega kwa bega kufanikisha mjadala huo wenye umuhimu mkubwa kwa ustawi wa watoto katika jamii ya Shinyanga.

Mjadala huu umeibua hoja nzito kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto ikiwemo ukatili wa kingono, ndoa za utotoni, kazi ngumu zisizolingana na umri, ukosefu wa elimu bora, pamoja na migogoro ya kifamilia ambayo huathiri moja kwa moja malezi na makuzi yao.

Wadau wamehimiza kuanzishwa kwa mikakati endelevu ya utoaji elimu kwa jamii kuhusu malezi chanya, huku wakitoa rai kwa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuongeza nguvu katika kulinda haki za watoto.

Kwa kauli moja, washiriki wa mdahalo huu wameafiki kuwa hatima ya mtoto wa leo ndiyo msingi wa taifa la kesho, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha mtoto analelewa kwa maadili, upendo na ulinzi unaostahili.

Afisa Mradi kutoka ICS, Bi. Lucy Maganga akizungumza kwenye mjadala maalum kuhusu malezi na makuzi ya mtoto ambao umefanyika katika ukumbi wa Radio Faraja leo Julai 9, 2025.




Post a Comment

Previous Post Next Post