Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kupitia Idara ya Mifugo, inaendelea kutekeleza zoezi la uchanjaji wa kuku kama sehemu ya mkakati wa kudhibiti na kutokomeza magonjwa hatari yanayoathiri sekta ya ufugaji.
Zoezi hili ambalo ni awamu ya kwanza ya mpango wa chanjo kwa mifugo, linahusisha utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya kideri, ndui, na mafua makali ya kuku.ambapo leo Julai 9, 2025, zoezi hili limeendelea kutekelezwa katika Kata ya Ngokolo na Kata ya Ibadakuli, ambapo wafugaji wa kuku wamejitokeza kwa wingi kuhakikisha mifugo yao inalindwa dhidi ya milipuko ya magonjwa hayo.
Wakizungumza kuhusu chanjo hizo, baadhi ya wafugaji wameipongeza serikali kwa kuwapatia chanjo za ruzuku huku wakieleza kuwa hatua hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kuboresha afya ya mifugo yao. kwani ufugaji wa kuku umekuwa chanzo muhimu cha kipato,pamoja na fursa za ajira kwa vijana waliopo katika jamii zao.
Zoezi la uchanjaji huu linaendelea kutolewa bila malipo katika Manispaa ya Shinyanga, ambapo lilianza rasmi Julai 7, 2025, na linatarajiwa kuendelea kwa muda wa wiki mbili likihusisha kata zote 17 za halmashauri ya manispaa ya Shinayanga.
Hatua hii inaakisi dhamira ya Serikali katika kuboresha sekta ya mifugo, kukuza uchumi wa kaya, na taifa kwa ujumla ambapo manispaa ya Shinyanga inaendelea kuwahamasisha wafugaji wote kushiriki kikamilifu ili kufanikisha azma ya serikali ya kuondoa kabisa vifo vya mifugo vinavyotokana na magonjwa yanayozuilika.
Post a Comment