" MWANAMKE MWENYE ULEMAVU MWAJUMA MBOGO AREJESHA FOMU YA UDIWANI NGOKOLO, ASEMA YUPO TAYARI KUITENDEA HAKI RIDHAA YA CCM

MWANAMKE MWENYE ULEMAVU MWAJUMA MBOGO AREJESHA FOMU YA UDIWANI NGOKOLO, ASEMA YUPO TAYARI KUITENDEA HAKI RIDHAA YA CCM

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwanamke jasiri na mwenye ulemavu, Mwajuma K. Mbogo, leo Julai 1, 2025, ameendeleza dhamira yake ya kisiasa kwa kurejesha rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania nafasi ya udiwani katika Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga.

Mwajuma, ambaye alichukua fomu hiyo Juni 29, 2025, amesema kurejesha fomu ni hatua rasmi ya kuthibitisha kwamba yupo tayari kwa ajili ya kutumikia wananchi wa Ngokolo endapo chama chake kitamuidhinisha.

"Nimerudisha fomu nikiwa na moyo wa shukrani na ujasiri. Nimeiva, nina uzoefu, na nina ari ya kuwa sehemu ya mabadiliko chanya kwa wananchi wa Ngokolo, hasa wanawake na watu wenye ulemavu," amesema Mwajuma mara baada ya kurejesha fomu.

Ameongeza kuwa hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kufunga Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyompa msukumo mkubwa wa kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho, kutokana na namna alivyohimiza usawa wa kijinsia na ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye nafasi za uongozi.

Kwa mujibu wa Mwajuma, uzoefu wake katika uongozi unampa ujasiri mkubwa. Ametaja nyadhifa mbalimbali alizowahi kushikilia, ikiwemo:

·         Mjumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii (tawi)

·         Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tawi la Mwadui (2015)

·         Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT tawi la Mwadui

·         Mwenyekiti Msaidizi wa CHAWATA Wilaya ya Shinyanga

·         Mjumbe wa SHIVYAWATA Wilaya ya Shinyanga Mjini

"Ulemavu si kikwazo. Tunahitaji kuamini uwezo wa mtu, si hali yake ya mwili. Nipo tayari kuitumikia Ngokolo kwa uaminifu, ushirikiano na uwazi," amesisitiza Mwajuma.

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya CCM linaendelea kote nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA


 

Post a Comment

Previous Post Next Post