Na Mwandishi wetu, Kahama
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, inatarajiwa kuupokea Mwenge wa Uhuru kimkoa Agosti 3, 2025 ukitokea mkoani Tabora, na kuanza kukimbizwa siku hiyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.
Mwenge wa Uhuru 2025 utapokelewa katika viwanja vya kituo cha mabasi Kagongwa ukitokea Tabora majira ya saa 12 kamili asubuhi ambapo wananchi wote wanakaribishwa kushuhudia zoezi hilo.
Hata hivyo shughuli mbalimbali zimeendelea ndani ya Manispaa ya Kahama ambayo ni mwenyeji kimkoa, ikiwa ni pamoja na viongozi pamoja na watumishi wa Manispaa kuendelea na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Miradi hiyo ni ile itakayofunguliwa na Mwenge wa Uhuru, itakayowekewa mawe ya msingi na itakayokabidhiwa tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Julai 26, 2025, akitembelea na kukagua miradi hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Ndugu Masudi Kibetu amesema, jumla ya miradi 7 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 6.4 itapitiwa na mbio hizo.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru kwani watapata fursa ya kuukimbiza na kuangazia miradi yao ya maendeleo iliyolenga kuwasogezea huduma karibu.
Mradi utakaokabidhiwa
Kibetu amesema katika mbio hizo, mradi 1 utakabidhiwa kwa kikundi cha vijana cha madereva wa pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) 10, zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 110.
Amesema pikipiki hizo ni matunda ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri, ambapo 4% inakwenda kwa wananwake, 4% kwa vijana na 2% ni kwa wenye ulemavu (4,4,2).
Aidha ameeleza kuwa Halmashauri yake imekuwa ikitekeleza kikamilifu takwa hili la kisheria, na kuyasisitiza makundi hayo kufika halmashauri kitengo cha maendeleo ya jamii, ili kupata utaratibu na kuweza kunufaika na mkopo huo kwani fedha bado zipo.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ilitoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.2 kwenda kwenye vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, kikiwemo kikundi hiki cha vijana wa bajaji Kagongwa.
Miradi itakayofunguliwa
Miongoni mwa miradi hiyo ni chumba cha maabara ya sayansi mchanganyiko iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 58.3 katika shule ya sekondari mama Kalembe iliyopo kata ya Mwendakulima, ambapo pia zitazinduliwa klabu za mazingira na ya wapinga rushwa.
Mradi mwingine ni mradi wa kituo cha uwekezaji wa kituo cha mafuta FRONT OIL eneo la Mhongolo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.92.
Miradi itakayowekewa mawe ya msingi
Mradi wa ujenzi wa jengo la uraibu wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 349.8.
Mradi mwingine ni wa ujenzi wa chujio la maji Mwendakulima wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.87, pamoja na ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 1.115 kwa kiwango cha lami, eneo la viwanda vya mpunga Kagongwa, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.08 ambayo ni mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mkesha wa Mwenge wa Uhuru 2025
Amesema eneo la mkesha wa Mwenge wa Uhuru katika Manispaa hiyo August 3, 2025, ni katika uwanja wa Magufuli na shughuli mbalimbali za kijamii zitakuwa zikiendelea ikiwemo upimaji wa ugonjwa wa malaria bure kwa wananchi wote.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2025, zinabeba kauli mbiu isemayo “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Ndugu Masudi Kibetu wa kwanza (kulia), pamoja na watumishi wengine wa Halmashauri, wakipokea maelezo kutoka kwa kikundi cha vijana cha madereva wa pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) 10, zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 110, katika kata ya Kagongwa, ambazo zitakabidhiwa na Mwenge wa Uhuru 2025.

Muonekano wa ndani wa maabara ya kisasa ya sayansi mchanganyiko katika shule ya sekondari mama Kalembe iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 58.3, ambao unatarajiwa kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru 2025.

Post a Comment