Na Mapuli Kitina Misalaba
Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Tanzania (TAWOSCO) unatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa Nne wa mwaka, tukio ambalo limepangwa kufanyika Julai 23, 2025 katika Hoteli ya Mwanza Lenana, kuanzia saa 2:00 asubuhi.
Mkutano huo muhimu unatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu kutoka mikoa yote ya Tanzania, huku ukiwa na lengo la kujadili maendeleo ya elimu nchini pamoja na changamoto zinazowakabili wamiliki wa shule na vyuo binafsi, hasa wanawake.
Mgeni rasmi katika mkutano huo atakuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ambaye anatarajiwa kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu sekta ya elimu pamoja na kusikiliza maoni ya wamiliki wa shule binafsi.
Aidha, mgeni mwalikwa maalum ni Peter Frank maarufu kama Mr. Black, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BSL Investment Co. Ltd, mwanzilishi wa The True Life Foundation pamoja na shule za BSL zilizopo Tanzania na Rwanda. Mr. Black anatarajiwa kutoa mada ya kuhamasisha wanawake wamiliki wa shule kuhusu ujasiriamali, uongozi na mabadiliko chanya katika elimu.
Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za TAWOSCO za kuwaunganisha wamiliki wa shule na vyuo nchini kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kuhamasishana, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuinua elimu bora inayoendana na mahitaji ya sasa ya kijamii na kitaifa.
Kwa mujibu wa waandaaji, wanachama wote wa TAWOSCO pamoja na wadau wa elimu wanakaribishwa kushiriki kwa wingi ili kuimarisha ushirikiano na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu nchini.
Post a Comment