Na, Egidia Vedasto,
Misalaba News, Arusha.
Vijana Jijini Arusha wamenolewa juu ya ulipaji wa kodi na kukumbushwa kuanzisha biashara kwa kufuata kanuni na raratibu ili wasije kukutana na vikwazo wakati wa uendeshaji.
Akitoa mafunzo ya Kodi yanayowezeshwa na Shirika la Okoa New Generation kwa kushirikiana na Restless Development kwa vijana Jijini Arusha, Afisa TRA Arusha Nicodemus Massawe amesema lengo la serikali ni kuona vijana wanaanzisha biashara kwa wingi na kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Amesema wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha biashara na wale wafanyabiashara wadogo wanatakiwa kusajiri biashara zao na kujenga utamaduni wa kutunza kumbukumbu ili kulinda biashara na mali isipotee.
"Lengo letu ni kutoa elimu kwa upana ili walipa kodi watambue haki zao na wapi pa kupata majibu ya maswali yao, na tunataka wafanyabiashara waongezeke hususan vijana, tunaahidi kuendelea kushirikiana nanyi kila mtakapohitaji msaada wetu" amesema Massawe.
Hata hivyo amefafanua kuhusu baadhi ya watendaji wasio na kauli ya ukarimu kwa wateja, ameahidi atahakikisha anazungumza nao ili wabadilike na kusaidia wateja wao badala ya kuwavunja moyo.
Miliana Charles ni mjasiliamali anayeuza pilipili, vitunguu swaum na maenbe yaliyokaushwa, kupitia mafunzo hayo amesema amenufaika na anatarajia kusajiri biashara yake na kufuata taratibu za kodi ili kuhakikisha biashara yake inakua na si kuzorota.
"Mwaka jana nilianzisha biashara lakini haikuendelea kwa sababu sikuwa na elimu ya biashara na kodi ninazotakiwa kulipa, na sikujua mimi ni mfanyabiashara wa aina gani, sasa baada ya elimu hii kutoka TRA kupitia shirika la Okoa New Generation na Restless Development nitafikia lengo la kuwa mfanyabiashara mkubwa,
"Watoa wa elimu kwa mteja kutoka mamlaka ya mapato na matumizi nchini TRA wametuhakikishia ushirikiano wa kina pale tutakapohitaji msaada wao, kwetu vijana ni hatua kubwa ya kumaliza changamoto za biashara" Amesema Miliana.
Katika namna hiyohiyo Mwenda Issa anayetarajia kuanzisha biashara hivi karibuni, ameahidi kulipa kodi ipasavyo ili kutimiza wajibu wake kama kijana na mzalendo kwa lengo la kuongeza mapato ya nchi na kuimarisha miradi mbalimbali.
Mratibu wa mradi wa "Kijana Wajibika Shiriki Kulipa Kodi Yako" unaotekelezwa na shirika la Okoa New Generation (ONG) Shaban James amesema ni furaha yake kuona vijana wake wanaendelea kupata mwangaza juu ya suala la kulipa kodi na wanapata hamasa ya kuanzisha biashara.
Amefafanua kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa na ndio wenye idadi kubwa nchini kwa takwimu za watu na makazi (NBS), hivyo wakielimishwa juu ya jambo lolote la kiuchumi itasaidia kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.
"Shukrani zangu za pekee ni kwa shirika la Okoa New Generation kwa kushirikiana na Restless Develepment pia watendaji wa mamlaka ya mapato na matumizi nchini (TRA) kutoka Arusha wameondoa dukuduku kwa vijana na kuwaeleza kuwa nia yao ni kuina kila mmoja anakua kiuchumi"amesema Shaban.
Post a Comment