Na Lucas Raphael,Tabora
Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC imewataka waratibu na wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi hususani vyama vya Siasa wavishirikishe katika vikao mbalimbali ili kuondoa malalamiko kuelekea uchaguzi mkuu wa octoba mwaka huu
Vyama vya siasa wanastahili kushirikishwa ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima ambayo hujitokeza wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa Jana na Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi INEC Kamishna Magdalena Rwebangira wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi ambayo yamewashirikisha zaidi ya maafisa 110 kutoka mikoa ya Kigoma na Tabora katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustino (AMUCTA) mkoani Tabora.
Alisema kwamba tume imewapatia dhamana ya kusimamia zoezi nyeti la uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani litakalokwenda kutoa mustakabali wa taifa hivyo ni muhimu kwao kuwa makini katika kutenda haki kwa mujibu wa katiba,sheria,kanuni na miongozo inayotolewa na Tume;
Hata hivyo Kamishna Magdalena aliwakumbusha washiriki hao kuwa wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa kisheria na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa ukaribu na vyama vya siasa pamoja na wadau wengine wa uchaguzi ili kuimarisha imani ya wananchi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
“Epukeni kusababisha taharuki au malalamiko kwa vyama vya siasa.Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba,Sheria,Kanuni,Miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,” alisema Kamishna Magdalena .
Kaulimbiu ya uchaguzi mkuu huo ni: “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura”, kauli inayolenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi wa ngazi zote kwa kutumia haki yao ya kikatiba.
Mwisho
Post a Comment