" MACHINGA TABORA: OKTOBA TUNATIKI KWA RAIS SAMIA

MACHINGA TABORA: OKTOBA TUNATIKI KWA RAIS SAMIA

Na Lucas Raphael,Tabora

 

SHIRIKISHO la Umoja wa Wamachinga (SHIUMA) Mkoani Tabora limempongeza Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanywa ikiwemo kuwajali wafanyabiashara ndogo ndogo nchini.

Tamko hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Mkoa wa Tabora Zuberi Omari alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwenye jengo lao jipya la Ofisi waliyojengewa na serikali ya awamu ya 6.

Alisema kuwa wamachinga wote wa Mkoa huo wameridhishwa na utendaji wa Rais Samia ikiwemo kuwatambua, kuthamini shughuli wanazofanya na kuwapa mikopo ya kuendeleza shughuli zao kupitia mapato ya halmashauri.

Alidokeza kuwa hatua ya Rais Samia kuagiza halmashauri zote nchini kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara na kuwawezesha mikopo isiyo na riba imewapa nguvu ya kufanya biashara zao kwa kujiamini na maisha yao kuinuka zaidi.

 ‘Rais Samia ameboresha shughuli zetu kwa kiasi kikubwa na amekuwa chachu ya mafanikio yetu, ndio maana tumeamua kuungana na kutoa tamko la pongezi na kumwahidi kuwa mwaka huu tutampigia kura za kishindo’, alisema.

Zuberi aliongeza kuwa serikali ya awamu ya 6 pia imewajengea ofisi mpya ya kufanyia shughuli zao na tayari wamekabidhiwa jambo ambalo limewapa faraja kubwa na kujiona kuwa wanathaminiwa sana.

Tuanatarajia kufanya makongamano makubwa 2 moja hapa Tabora na jingine Mkoani Kigoma ili kujengeana uwezo zaidi kama Shirikisho la Umoja wa Wamachinga na kuelezana fursa walizopewa na serikali ili wote wazichangamkie.

Mwenyekiti alibainisha kuwa fursa walizopewa na serikali ya Rais Samia zimekuwa chachu ya kuzalisha walipa kodi na kukuza mitaji yao na kuinuka juu zaidi, na sasa wamepatiwa vitambulisho watakavyovitumia kwa miaka 3 hivyo kuwa na fursa ya kukopeshwa na taasisi nyinghine za kifedha.

Alisisitiza kuwa SHIUMA sio taasisi ya kisiasa na haiamulishwi na mtu au chama chochote cha siasa juu ya ushiriki wake kupiga kura mwaka huu, hivyo akabainisha kuwa mwezi Oktoba mwaka huu watampigia kura Rais Samia.

 Alieleza kuwa kila mwananchi mwenye sifa ya kushiriki uchaguzi huo anayo haki ya kikatiba ya kupiga kura na kufanya maamuzi yake binafsi pasipo kupangiwa na chama ama mtu yoyote isipokuwa kwa utashi wake tu.

‘Hatuwezi kupangiwa na chama, sisi tutashiriki kikamilifu uchaguzi mwaka huu ili kutumia demokrasia yetu vizuri, hatuwezi kuwasikiliza wanaosema No Reform, No Election, sisi tuna maamuzi yetu, alisema’, alisema.

Awali akitoa salamu kwa wamachinga, Ofisa Manunuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kati na Magharibi Hussein Msumeno aliwataka kujiunga katika vikundi na kuomba zabuni za kufanya shughuli hizo ili kunufaika na fursa ya asilimia 30 iliyotengwa na serikali kupitia mfumo wa NeST. 

Msumeno alisema kuwa mfumo huo ni wa wazi na wa kisasa zaidi hivyo akawataka kujisajili kidigitali ili kunufaika na zabuni zote zinazotangazwa na serikali.

Mwisho.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post