" WATUHUMIWA 125 WAKAMATWA SHINYANGA, DAWA ZA KULEVYA, MAGARI NA PIKIPIKI ZA WIZI VYANASWA

WATUHUMIWA 125 WAKAMATWA SHINYANGA, DAWA ZA KULEVYA, MAGARI NA PIKIPIKI ZA WIZI VYANASWA

Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limekamata jumla ya watuhumiwa 125 wa makosa mbalimbali ya kijinai kufuatia oparesheni zilizofanyika kati ya Juni 27 hadi Julai 22, 2025, kwa lengo la kuzuia uhalifu na kuhakikisha usalama wa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi amesema kuwa pamoja na watuhumiwa hao, pia wamefanikiwa kunasa vielelezo mbalimbali vikiwemo dawa za kulevya aina ya bhangi gramu 2,261, pombe ya moshi lita 142, mirungi kilo 29, runinga saba, pikipiki 22, bajaji moja, redio nane, mabati 16, vitanda vinne na vipande 17 vya nondo.

“Kati ya pikipiki hizo, baadhi zimebainika kuwa za wizi huku nyingine zikikutwa hazina usajili. Jeshi linaendelea na oparesheni ili kuhakikisha uhalifu unadhibitiwa na jamii inabaki kuwa salama,” amesema SACP Magomi.

Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema kuwa jumla ya kesi 25 zimefanikiwa kutolewa hukumu mahakamani, ambapo miongoni mwao, washitakiwa wa kesi mbili za kulawiti wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, huku kesi mbili za ubakaji zikiishia kwa washitakiwa kupewa kifungo cha miaka 30 kila mmoja.

Aidha, washitakiwa wa makosa mengine kama wizi, kuvunja nyumba usiku, kujeruhi na shambulio la kudhuru mwili wamehukumiwa vifungo vya kuanzia miezi miwili hadi miaka minne, huku wengine wakipewa adhabu kwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Kwa upande wa usalama barabarani, Kamanda Magomi amesema kuwa kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, jumla ya makosa 5,759 yamekamatwa, ambapo 4,557 ni ya magari na 1,202 ni ya bajaji na pikipiki. Madereva walioshikiliwa wamelipia faini papo kwa hapo, huku madereva watatu wakifungiwa leseni kwa miezi mitatu kwa kuendesha kwa kasi ya zaidi ya kilomita 100 kwa saa.

Jeshi hilo pia limefanikiwa kufanya mikutano 64 ya kutoa elimu ya usalama kwa wananchi, shule, taasisi za dini, vikundi vya ulinzi shirikishi na kwenye vituo vya usafiri, hali iliyosaidia kupunguza makosa ya ukatili wa kijinsia na uhalifu kwa ujumla.

Kamanda Magomi amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kupambana na uhalifu na kutoa wito kwa wote kuendelea kutii sheria, kanuni na taratibu ili kudumisha hali ya amani na utulivu mkoani humo.

Post a Comment

Previous Post Next Post