" RAIS DKT. SAMIA: TANZANIA YAONGOZA KWA AMANI AFRIKA MASHARIKI

RAIS DKT. SAMIA: TANZANIA YAONGOZA KWA AMANI AFRIKA MASHARIKI




Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan akimtambulisha mgombea Mwenza Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi wakati akizindua kampeni za chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es Salaam Agosti 28, 2025.

……………….

Na John Bukuku, Dar es Salaam

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imeendelea kuwa kinara wa amani na utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki, hatua inayotokana na mshikamano wa kitaifa na uongozi imara wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 uliofanyika leo kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, Dkt. Samia alisema Tanzania imepata heshima kubwa kimataifa kutokana na kulinda misingi ya amani, muungano, uhuru na mshikamano wa wananchi wake.

“Tanzania inaongoza kwa viwango vya amani ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki. Tumefanikiwa kuimarisha Muungano, kulinda uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar, na kudumisha mshikamano wa kitaifa. Haya yote yametuwezesha kuendelea kuwa taifa lenye heshima na mshikamanifu,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu sio wa kuchagua viongozi pekee, bali ni fursa ya Watanzania kuendeleza safari ya kuinua hali ya maisha, kukuza ustawi wa jamii na kujenga taifa imara linalojitegemea.

Dkt. Samia alitumia fursa hiyo kushukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumchagua kupeperusha bendera ya chama hicho na kwa kuridhia pendekezo la mgombea mwenza wake, Balozi Emmanuel Nchimbi.

Akizungumzia sekta ya habari, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeimarisha uhuru wa vyombo vya habari kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Habari ya mwaka 2016 na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikiyakandamiza magazeti mbalimbali.

“Serikali imetoa leseni zaidi ya 1,000 kwa magazeti na majarida, redio, televisheni na vyombo vya habari mtandaoni. Huo ndio ushahidi wa uhuru wa vyombo vya habari tulionao leo,” alisema.

Kwa upande wake, Mgombea Mwenza, Balozi Emmanuel Nchimbi, alisema yupo tayari kushirikiana na chama na mgombea urais kuhakikisha ushindi wa CCM na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

“Nipo tayari na timamu kutekeleza maelekezo ya chama chetu katika kutafuta ushindi, na baadaye kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo,” alisema.


GUSA LINK HAPA CHINI👇


APPLICATION FORM

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

 





Post a Comment

Previous Post Next Post