
Na Mapuli Kitina Misalaba, Picha zote na Kadama Malunde
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Itwangi kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Azza Hillal Hamad, ameweka bayana vipaumbele vyake vya
maendeleo, akiahidi kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha changamoto
zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza, katika uzinduzi wa kampeni uliohudhuriwa
na maelfu ya wananchi na viongozi wa CCM, Azza amesema dhamira yake kubwa ni
kuhakikisha huduma za kijamii kama afya, maji, kilimo na miundombinu ya
barabara zinaboreshwa kwa kiwango kikubwa ili kuinua ustawi wa wananchi.
“Nimekuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa vipindi viwili.
Mnanifahamu mimi si mtu wa kupindapinda, mimi ni mtu wa kusema ukweli na
kuchukua hatua. Naomba mnitumie, nitahakikisha huduma za afya zinaboreshwa na
kukamilisha zahanati na vituo vya afya ambavyo bado havijakamilika, ikiwemo Manyada,
Nyida na Butini,” amesema Azza
Akizungumzia sekta ya kilimo, Azza amesema kilimo
ndicho uti wa mgongo wa Jimbo la Itwangi, hasa kilimo cha mpunga, na akaahidi
kupigania kukamilika kwa Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida na miradi mingine ya
kilimo inayosuasua.
“Jimbo la Itwangi lina fursa kubwa za kilimo, lakini
miradi mingi ya umwagiliaji haijakamilika. Naomba mniamini, nitasimama
kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa maslahi ya wakulima na taifa kwa
ujumla,” alisema Azza.
Kwa upande wa maji, Azza amesema serikali ya Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan tayari imetekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa
Victoria, lakini bado kuna vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.
“Kuna vijiji 22 vinavyopitiwa na Mradi wa Maji wa Tinde Package ambavyo bado
havijapata maji, ikiwemo Kata ya Usanda. Nikichaguliwa, nitahakikisha vijiji
hivyo vinapata huduma ya maji safi na salama,” ameahidi Azza.
Azza amewaomba wananchi wa Itwangi kujitokeza kwa
wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kupiga kura na kuhakikisha ushindi wa CCM kuanzia
ngazi ya Udiwani, Ubunge hadi Urais.
“Naomba mnipigie kura ili niwatumikie kwa uadilifu na kuhakikisha kila mradi wa
maendeleo unakamilika. Pia tumuunge mkono Rais wetu mama Dkt. Samia Suluhu
Hassan na madiwani wetu wote wa CCM,” alisema.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM, Munde Tambwe Abdalla, amesema wananchi wa Itwangi
wamepata kiongozi sahihi kwa sababu Azza ni jasiri, mjenga hoja na mtetezi wa
wananchi.
“Nawaomba wananchi wa Itwangi, Oktoba 29 mpigie kura Azza Hillal, Rais Dk.
Samia na madiwani wote wa CCM ili Jimbo la Itwangi lipate maendeleo ya haraka,”
alisema Munde.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amesema
Azza ni mchapakazi na mwenye uchungu wa kweli kwa maendeleo ya wananchi, huku Mwenyekiti
wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Edward Ngelela, akisisitiza kuwa chama kina imani
kubwa na mgombea huyo kutokana na utendaji wake wa kazi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wameeleza
imani yao kwa Azza, wakisema historia yake ya utendaji kazi na kupigania
maslahi ya wananchi tangu akiwa Mbunge wa Viti Maalum imewavutia kumchagua.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utafanyika Oktoba 29, ambapo wananchi watawachagua
madiwani, wabunge na Rais.
Kampeni zimeanza rasmi na CCM inaendelea kusisitiza sera zake za maendeleo
kupitia viongozi wake na wagombea katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Post a Comment