" MAHAFALI YA 17 YA SHULE YA MSINGI LUBAGA YAFANA, MKURUGENZI WA SHUWASA AHAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO

MAHAFALI YA 17 YA SHULE YA MSINGI LUBAGA YAFANA, MKURUGENZI WA SHUWASA AHAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO


Na Mapuli Kitina Misalaba


Shule ya Msingi Lubaga, iliyopo Manispaa ya Shinyanga, leo Septemba 19, 2025 imefanya mahafali yake ya 17 kwa wahitimu 64 wa elimu ya msingi, ambapo hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, walimu, wazazi, wanafunzi na wageni waalikwa.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) ambaye amewakilishwa na Afisa Uhusiano wa Umma wa SHUWASA, Nsianel Gerald, ambaye amewapongeza wahitimu kwa hatua kubwa waliyofikia na walimu kwa malezi na juhudi walizowekeza katika kuwafundisha na kuwalea watoto hao.

Kwa mujibu wa mkuu wa shule hiyo Mwalimu Stella Lucas Halimoja amesema Shule ya Msingi Lubaga imeendelea kuwa kinara wa taaluma katika Manispaa ya Shinyanga ambapo tangu mwaka 2018 hadi sasa, shule imekuwa ikifaulisha kwa kiwango cha juu cha kati ya asilimia 99 hadi 100, na kwa miaka minne mfululizo (2021–2024) imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kati ya shule za serikali katika Manispaa.

Amesema mwaka 2018 wanafunzi 73 walihitimu na wote kufaulu kwa asilimia 100, huku mwaka 2024 wanafunzi 65 pia walihitimu kwa ufaulu wa asilimia 100 na shule kushika nafasi ya kwanza kiwilaya.

Mwalimu Halimoja ameeleza kuwa matokeo hayo, yamechangiwa na nidhamu, majaribio ya kila wiki, na mipango ya shule ya kuhakikisha wanafunzi wanajifunza kwa bidii na kujituma.

Mbali na taaluma, shule imefanikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo:

Mpango wa Chakula: Shule imeanzisha mpango wa kupika chakula na uji shuleni, hatua iliyoimarisha utulivu wa wanafunzi darasani.

Stella amesema Wanafunzi wa madarasa ya mitihani wamekuwa wakifanya majaribio kila wiki, jambo lililowasaidia kuongeza uelewa na kujiandaa vizuri kwa mitihani.

Ametumia nafsi hiyo kueleza mafanikio mbalimbali katika shule hiyo ikiwemo kufanikisha Ujenzi wa choo cha walimu, choo cha wasichana chenye matundu matano, chumba cha kujihifadhi kwa wanafunzi wa kike, na vyumba viwili vya madarasa.

Aidha amesema kupitia kamati ya shule na Ofisi ya Diwani, jamii imesaidia kukamilisha ujenzi wa madarasa mapya yaliyokamilika kwa asilimia 85, pia Shule imepata mashine ya kudurufu nyaraka kupitia msaada wa mlezi wa shule, Ndugu Gillio Makula, hatua iliyorahisisha utoaji wa mitihani na majaribio.

Pamoja na mafanikio hayo, shule inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukosefu wa madirisha ya vioo na viti kwenye ofisi ndogo ya shule, uchakavu wa nyumba ya mwalimu, na hitaji la upakaji rangi kwenye baadhi ya majengo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa SHUWASA, Afisa Uhusiano wa Umma Nsianel Gerald, ameipongeza shule hiyo kwa mafanikio makubwa na nidhamu ya wanafunzi na walimu.

Amesema, SHUWASA itaendelea kushirikiana na shule katika kutatua changamoto zilizopo, ikiwemo kusaidia maboresho ya miundombinu na mazingira ya kufundishia.

“Sisi kama SHUWASA tutawawekea madirisha ya Vioo, Meza na viti vyake”amesema Nsianel

Wahitimu wakiwasili kwa ajili ya kuanza sherehe yao.

Wahitimu wakiwasili kwa ajili ya kuanza sherehe yao.

Mkuu wa shule ya msingi Lubaga Mwalimu Stella Lucas Halimoja, akizungumza kwenye mahafali ya 17 leo Septemba 19, 2025.





 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post