" MLINZI AUAWA NA WATU WASIOJULIKANA SHINYANGA MJINI, POLISI WAMSHIKILIA MTUHUMIWA MMOJA

MLINZI AUAWA NA WATU WASIOJULIKANA SHINYANGA MJINI, POLISI WAMSHIKILIA MTUHUMIWA MMOJA



Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Juma Mpuya mwenye umri wa Miaka 45, mlinzi wa maduka ya mfanyabiashara amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana katika eneo lake la kazi Mjini Shinyanga.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Septemba 17, 2025, katika mtaa wa Majengo Mapya, kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mwili wa marehemu ulikutwa umefungwa sehemu za mikono na miguu na kuwekwa chini, huku baadhi ya mali zilizokuwa dukani zikidaiwa kuibiwa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtaa wa Majengo Mapya, Bwana. Philimon Chikala, ameeleza kupokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa wananchi na kufika eneo la tukio kwa ajili ya hatua za awali.

Akizungumza na Misalaba Media, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa jeshi la polisi limeanza uchunguzi wa kina.

“Ni kweli tukio hili limetokea, na tunashikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano. Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Kamanda Magomi.

Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu na kuimarisha usalama katika mkoa huo.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post