Na Osama Mohamedi Chobo, Misalaba Media-kilwaMkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amezindua rasmi kisima cha maji kilichojengwa katika Kijiji cha Mtepera kwa gharama ya shilingi milioni 46, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mipango endelevu ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Nyundo alielekeza Wakala wa Maji Vijijini na Mijini (RUWASA) kuhakikisha kuwa kisima hicho kinakuwa chachu ya usambazaji wa maji kwa maeneo mengine ya kijiji, akieleza kuwa kisima hicho pekee hakiwezi kutosheleza mahitaji yote ya wananchi.> “RUWASA wahakikishe wanapanua huduma hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Kisima hiki ni hatua nzuri, lakini hatupaswi kukomea hapa. Maji yafike kwenye maeneo ya msingi kama shule, zahanati na kaya nyingi zaidi,” alisema DC Nyundo.Aidha, aliwataka RUWASA kuwasiliana na wadau wa TACHA – Chama cha Uhifadhi wa Mazingira na Wawindaji wa Asili Tanzania – kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina juu ya uwezo wa kisima hicho kuhudumia wakazi wa Mtepera kwa ufanisi.Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza pia umuhimu wa kuwa na mpango wa matengenezo endelevu wa mradi huo, ili pale changamoto zitakapojitokeza ziweze kutatuliwa kwa haraka bila kusitisha huduma ya maji kwa wananchi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TACHA, Thomas Ndonde, alieleza namna walivyobaini changamoto ya upatikanaji wa maji katika kijiji hicho na kuamua kushirikiana na wadau wengine kutafuta suluhisho.> “Tuliona namna wananchi wa Mtepera walivyokuwa wakiteseka kutokana na ukosefu wa maji. Kupitia ushirikiano wa TACHA na wadau wengine, tumeweza kuanza kutatua tatizo hili kwa vitendo,” alisema Ndonde.Mradi huo wa maji unatarajiwa kunufaisha mamia ya wakazi wa kijiji cha Mtepera, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya uhaba wa maji safi na salama.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment