





…………
Na Munir Shemweta, WANMM
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amewataka waajiriwa wapya wa Wizara hiyo kuwa wabunifu sambamba na kuwajibika ipasavyo ili kuboresha utendaji kazi katika maeneo waliyopangiwa.
Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo tarehe 18 Septemba 2025 wakati wa Mafunzo ya Awali kwa waajiriwa wapya 312 watakaohudumu katika kada mbalimbali.
‘’Kila mmoja wenu atafakari kufanya ubunifu kwenye eneo lake la kazi alilopangiwa, lengo hapa ni kuboresha utendaji kazi katika kutoa huduma kwenye sekta ya ardhi’’ amesema Mhandisi Sanga.
Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewaasa watumishi hao wapya kuwajibika ipasavyo kwa kuzingatia kazi iliyokusudiwa, muda na ubora wa kazi waliyopangiwa.
‘’Lazima muwajibike kikamilifu mpaka bosi wako akupende kutokana na kufanya kazi kwa ubora na kwa muda uliopangiwa, muwe sehemu ya mafanikio ya Wizara’’ amesema.
Vile vile, Mhandisi Sanga amewataka watumishi hao, kuwa na mahusiano mazuri kazini na kuacha kujitenga kwa kuwa maeneo ya kazi yanahitaji utendaji kazi wa pamoja. Aidha, amewasisitizia umuhimu wa kutunza siri za serikali wakati wote wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika maeneo ya kazi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera amewakaribisha watumishi hao wapya na kuwaeleza kuwa wamepata bahati kubwa ya kufanya kazi Wizara inayohudumia watu wote na ambapo amewataka kuzingatia haki, utu na uwajibikaji wakati wanapohudumia wananchi.
‘’Fursa mliyoipata mkaitumie kwa uadilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma wakati wote wa kutekeleza majukumu yenu’’ amesema Lucy.
Post a Comment