
Utaratibu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara kati ya Sekta za Umma na Binafasi sio tu ni nguzo muhimu ya ukuaji wa biashara na uwekezaji, bali pia ni msingi imara wa utawala bora, uongozi unaozingatia watu na maendeleo endelevu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati anafungua kikao kati ya Watendaji Wakuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (East African Business Council – EABC) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika jijini Dar Es Salaam Septemba 16, 2025.
Waziri Kombo ameelezea matumaini yake kuhusu umuhimu wa vikao vya namna hiyo katika kupambanua changamoto zinazozikabili sekta binafsi nchini na kupendekeza mikakati inayotekelezeka ya kuinua biashara, ushindani na kufungua fursa kwa jamii ya wanyabiashara nchini Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Waziri Kombo ameendelea kwa kukitaka kikao hicho kujadili mchango wa sekta muhimu kama vile kilimo, viwanda, uchukuzi na biashara za mipakani ambazo zimekuwa zikikumbwa na vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha ustawi wake, akiitaja sekta ya wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) ni muathirika mkubwa wa vikwazo hivyo.
Amesema vikwazo visivyo vya kiforodha vimendelea kuwa moja ya kikwazo kikuu kinachorejesha jitihada za wanajumuiya wa EAC kuchangamkia fursa kama ilivyotarajiwa na waasisi wa Jumuiya ya kuwa na soko la pamoja kubwa kwa kuruhusu ufanyaji huru wa biashara ya bidhaa na huduma pamoja na mitaji ambavyo ni vigezo vitakavyoitambulisha jumuiya kama eneo muhimu na bora la biashara na uwekezaji.
Waziri Kombo amehitimisha hotuba yake kwa kuuhakikishia umma kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati ya kutekeleza Sera zinazolenga kuboresha mazingira ya biashara, kukuza ushindani na ukuaji jumuishi wa uchumi ndani ya Jumuiya.






🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment