" Wamiliki wa Silaha Haramu Wapewa Siku 60 Kuzisalimisha

Wamiliki wa Silaha Haramu Wapewa Siku 60 Kuzisalimisha

 

Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza msamaha wa miezi miwili kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, ambapo watalindwa dhidi ya mashitaka endapo watasalimisha silaha hizo kwa hiari kuanzia Septemba 1 hadi Oktoba 31, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, DCP David Misime, msamaha huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, kwa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 66 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, Sura ya 223 na marejeo ya mwaka 2023.

“Serikali imetoa msamaha wa kutoshitakiwa kwa wamiliki wa silaha kinyume cha sheria endapo watasalimisha silaha haramu kwa hiari kuanzia tarehe 01/09/2025 hadi 31/10/2025, kama ulivyotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 537 la tarehe 29/8/2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi limefafanua kuwa usalimishaji utafanyika nchi nzima, katika vituo vya Polisi, ofisi za Serikali za Mitaa, au kwa watendaji wa kata na shehia kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.

Msemaji wa Polisi ameongeza kuwa, yeyote atakayesalimisha silaha ndani ya kipindi cha msamaha “hatachukuliwa hatua zozote za kisheria”, lakini akatahadharisha kuwa, “mtu yeyote atakayepatikana na silaha baada ya kipindi cha msamaha atakamatwa na kuchukuliwa hatua zingine za kisheria.”

Msamaha huo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuhusu udhibiti wa silaha ndogo na nyepesi, ambayo yameeleza kuwa uzagaaji wa silaha haramu umeendelea kusababisha uvunjifu wa amani, vifo, majeruhi na hofu kwa wananchi.

Jeshi la Polisi pia limezitaka kampuni binafsi za ulinzi ambazo zimekuwa zikikodisha au kuazimisha silaha kinyume cha sheria kusitisha mara moja tabia hiyo na kuhakikisha silaha zinazotumika kiholela zinarudishwa kwa wamiliki au kusalimishwa katika kipindi hiki cha msamaha.

Aidha, wananchi ambao ndugu zao walimiliki silaha kihalali lakini wamefariki wametakiwa kuzisalimisha silaha hizo kulingana na masharti yaliyotolewa.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post