" WANAFUNZI 41,463 KUANZA MTIHANI WA DARASA LA SABA KESHO MKOANI SHINYANGA

WANAFUNZI 41,463 KUANZA MTIHANI WA DARASA LA SABA KESHO MKOANI SHINYANGA


Na Mapuli Kitina Misalaba


Maandalizi ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kwa mwaka 2025 yamekamilika mkoani Shinyanga, huku jumla ya watahiniwa 41,463 wakitarajia kuanza mtihani huo kesho Jumatano, Septemba 10, na kuhitimishwa siku ya Alhamisi, Septemba 11, 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia masuala ya elimu na mafunzo ya ufundi, Samson Hango, amesema mtihani huo unatarajiwa kufanyika katika halmashauri zote sita za mkoa huo ambazo ni Kahama Mjini, Kishapu, Msalala, Shinyanga Manispaa, Ushetu na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Amesema mkoa una jumla ya shule 664 zenye watahiniwa wa darasa la saba, ambapo kati ya hizo shule 598 ni za serikali na shule 66 ni zisizo za serikali.
Hango amebainisha kuwa jumla ya watahiniwa ni 41,463, wakiwemo wavulana 17,525 na wasichana 23,938, ambapo asilimia 94.53 wanatoka katika shule za serikali na asilimia 5.47 katika shule zisizo za serikali.

"Hadi kufika leo maandalizi yote yamekamilika, hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza. Tunategemea mtihani uende vizuri kwa siku zote mbili," amesema Hango.

Aidha, Hango amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwahimiza wanafunzi na kuwatia moyo ili waweze kufanya vizuri kwenye mtihani huo na kuendelea na hatua inayofuata ya elimu.

Misalaba Media imezungumza na baadhi ya wanafunzi kutoka shule za manispaa ya Shinyanga, ikiwemo Shule ya Msingi Mwenge, wamesema wako tayari kwa ajili ya mtihani huo kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya.


Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwenge, Esther Mbai  ameeleza kuwa walimu wamefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanafunzi wao wanafanya vizuri kwenye mtihani huo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia masuala ya elimu na mafunzo ya ufundi, Samson Hango, akizungumza na waandishi wa habari.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

 

Post a Comment

Previous Post Next Post