
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wameanza kwa kishindo katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3 – 0 dhidi ya Wiliete SC ya Angola. Mchezo huo umechezwa, Septemba 19, 2025, kwenye Uwanja wa Estádio 11 de Novembro, nchini Angola.
Yanga walitawala mchezo kuanzia dakika za mwanzo na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 31 kupitia kwa Aziz Andambwile, aliyepiga shuti kali kutoka nje ya eneo la hatari (18), shuti ambalo lilimshinda kipa wa Wiliete SC na kutinga wavuni.
Bao la pili la Yanga lilifungwa dakika ya 72 na Edmund John, aliyemalizia pasi murua kutoka kwa Maxi Nzengeli, baada ya kuwatoka walinzi wa Wiliete na kuweka mpira kimiani kwa ustadi mkubwa.
Dakika ya 82, mshambuliaji hatari wa Yanga SC, Prince Dube, aliifungia timu yake bao la tatu akiwa ndani ya eneo la 18, baada ya kupokea pasi safi na kumtoka beki kabla ya kuachia shuti lililomshinda kipa wa wenyeji.
Yanga SC sasa watarejea nyumbani kujiandaa kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo katika dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Post a Comment