
Klabu ya Yanga SC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC, katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa leo, Septemba 16, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkubwa ulivutia maelfu ya mashabiki kutoka pande zote mbili, huku kila timu ikionyesha kiwango cha juu cha maandalizi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa katika dakika ya 57 ya kipindi cha pili na mshambuliaji hatari wa Yanga, Pacome Zouzoua, goli ambalo liliamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa wamejazana kwa wingi uwanjani.
Kwa ujumla, mchezo ulikuwa wa kuvutia na wenye kasi, huku timu zote mbili zikibadilishana mashambulizi na kuonyesha mbinu mbalimbali za kiufundi.
Simba SC walitafuta bao la kusawazisha kwa nguvu lakini ukuta wa Yanga, ukiongozwa na kipa Djigui Diarra na mabeki wao imara, uliweza kudhibiti hatari zote.
Mchezo huu wa Ngao ya Jamii hutumika kama utangulizi rasmi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na ushindi huu unaipa Yanga SC hamasa kubwa kuelekea kampeni za msimu wa 2025/2026. Kwa ushindi huo, Yanga SC wanatwaa Ngao ya Jamii na kuendelea na kurekodi nzuri kuifunga Simba SC katika michezo sita hivi karibuni.
Post a Comment