Na Mchambuzi Maalum
SAUTI za kampeni za uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani nchini Tanzania zimechanganyikana na mvumo wa ajabu unaotoka katika mitandao ya kijamii, ukiongozwa na mwanamke anayeishi nchi za mbali.
Huyu si mwingine bali Mange Kimambi, Mtanzania anayeishi nchini Marekani, ambaye kwa muda mrefu biashara yake imejengwa katika kuuza maudhui yenye kejeli, dharau, na matusi dhidi ya watu maarufu, wasanii, na sasa, wanasiasa.
Mageuzi ya ajenda ya Mange yamefikia kilele chake wakati alipoamua kuelekeza mashambulizi yake ya maneno moja kwa moja kwa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kinachotia shaka zaidi katika dhamira yake dhaifu ni ile hali yay eye kufikia hatua ya kuanza kuhamasisha vijana kuandamana kwa nia ya kuitaka Serikali iondolewe madarakani kwa nguvu, na hata kutoa kauli zenye lengo la kukivuruga Jeshi la Ulinzi kumtii yeye badala ya utaratibu uliowekwa na Katiba ya nchi.
Hili si jambo dogo, ni mkondo wa hatari unaopaswa kuzingatiwa na kila Mtanzania anayethamini amani.
Biashara ya Mdomo Inayokula Bilioni
Kinachoshangaza zaidi ni ukweli kwamba uchochezi huu umefanywa kuwa biashara yenye faida kubwa. Inakadiriwa kuwa biashara hii ya uchochezi inamuingizia Mange Kimambi zaidi ya Shilingi Bilioni 1.5 kila mwezi.
Utajiri huu unatokana na wafuasi wake zaidi ya milioni moja wanaolipa kiasi cha Shilingi 1,500 kwa mwezi ili kupata fursa ya kusoma maudhui yake yanayolenga kudhalilisha.
Mbali na michango ya moja kwa moja kutoka kwa wafuasi, Mange ananufaika na wadhamini na wafadhili ambao wanapata faida kutokana na chuki, dharau, na kejeli anazotoa dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Hii ni biashara ya hatari ambayo inalisha chuki ndani ya jamii na kugharimu heshima ya taifa kwa maslahi binafsi.
Wito kwa Vijana: Amani ni Jasho, Sio Kelele
Ni muhimu kwa Watanzania, hasa vijana wanaomfuatilia Mange Kimambi, kuelewa ukweli mmoja wa msingi: amani haipatikani kwa kelele za matusi au kwa maneno matamu ya uchochezi; inalindwa kwa vitendo. Amani ya Tanzania imejengwa kwa gharama kubwa—kwa damu na jasho la wazalendo waliojitolea kulinda umoja.
Walinzi halisi wa amani leo ni vijana wanafanya kazi kwa bidii shambani, viwandani, na ofisini—sio wale wanaotafuta utajiri kwa kuwasha moto wa vurugu kutoka nchi za mbali.
Tanzania bado haijafika katika hali ya nchi zilizoporomoka kimaadili na kiuchumi kwa sababu ya fujo na maandamano yasiyo na msingi. Tunayo mifano ya nchi jirani ambako leo watumishi wa umma hawalipwi mishahara, huduma za afya zimekufa, na wawekezaji wamekimbia kutokana na machafuko ya kisiasa.
Tanzania bado inasimama imara, ina utulivu, na ina matumaini makubwa. Tusikubali kamwe kiongozi anayeishi Marekani kwa zaidi ya miaka 15, asiyeweza hata kukanyaga ardhi ya Tanzania kutokana na kesi zake za kudhalilisha, atuhubirie namna ya "kuikomboa nchi" huku yeye mwenyewe hajui hata bei halisi ya unga huko Kariakoo. Wakati huu wa uchaguzi, busara na utulivu ni ngao yetu kuu.

Post a Comment