Na Mwandishi wetu
Dereva wa malori anayejitambulisha kama Sudi Manyangari, amechukua jukwaa la mtandao wa kijamii wa TikTok na kutoa simulizi nzito, yenye kutisha, akilenga kuwaambia Watanzania umuhimu wa kulinda amani yao kwa gharama yoyote.
Manyangari, ambaye amejitaja kuwa mmoja wa watetezi wa amani nchini, anasema video yake imelenga kuamsha umma kwa vitendo, si kwa maneno matupu.
Katika video hiyo iliyoteka hisia za wengi, Manyangari alisimulia kisa kimoja cha safari zake za usafirishaji wa mizigo nchini Kongo DRC. Alieleza jinsi alivyopita mji iliyobaki mahame akiwa anaelekea eneo la wa Kongo la Beni kwa kupitia mpaka wa Kasindi nchini Uganda.
"Nimeona kutia uzito hili nikupeni kisa kimoja. Mimi nilipita miji kadhaa ya Kongo... la ajabu unakuta miji mikubwa kabisa, miji ambayo kama Kibaha ninapoishi mimi, mji una kila kitu, lakini miji imefungwa, hakuna watu. Nyumba zimefungwa, hakuna mnyama," alisema Manyangari.
Sehemu ya kutisha zaidi ya simulizi hiyo ni anavyoelezea hali aliyoikuta barabarani: "Barabarani unakutana na maiti za wanaume na wanawake zimekatwa vichwa."
Manyangari alieleza jinsi alivyojikuta peke yake bila utingo (turnboy), akijawa na hofu kali kwa mazingira hayo akitamani kuruka na kukimbia.
Anasema alikwama katika mlima, na kusaidiwa kuondoka katika mlima huo na madereva waliokuwa wanasafirisha shehena kutoka Mombasa.
Dereva huyo alisema kuwa hali hiyo ya machafuko aliyoshuhudia, ambayo anasema ni kama umetembea katika maafa ni mfano mdogo tu wa namna hali inavyokuwa amani inapotoweka.
Ujumbe huu mzito unawahimiza Watanzania kuthamini na kulinda amani yao, wakichukua funzo kutoka kwa hali mbaya ya nchi majirani.
Post a Comment