Na Lydia Lugakila, Misalaba Media
Mbeya
Mchungaji Thobias Tambikeni wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Forest ya Kwanza amewasisitiza waumini kumpenda Mungu na kuwapenda watu, huku akiwahimiza kuacha majivuno na kuishi maisha ya unyenyekevu.
Akizungumza na waumini wake wakati wa ibada iliyofanyika kanisani hapo Oktoba 26,2026.
Mchungaji Tambikeni amesema kuwa maisha ya duniani ni ya muda mfupi, hivyo ni muhimu kila mtu kujiandaa vyema kwa safari ya milele ambapo Kwa sasa watu wanatakiwa kuishi maisha ya kumjua Mungu na kupendana bila kubaguana
Amesisitiza kuwa, kwa kuwa dunia ni ya mpito, kila mwamini anatakiwa kutumia muda wake vizuri kwa kumtumikia Mungu kwa bidii na uaminifu.
Ameongeza kuwa, "Watu wenye kesi kesi ni wengi, lakini nguvu ya kumtumikia Mungu kwa bidii humfanya Mungu mwenyewe kushughulika na watu wake kwa nguvu na neema."
Katika mahubiri hayo, Mchungaji Tambikeni aligusia pia changamoto zinazowakabili wanandoa na waumini wengi kwa ujumla na kuwa watu wengi wa sasa nafasi yao ya kumjua Mungu ni finyu, na wanakwepa mafundisho yanayojenga wokovu wa kweli.
"Kinachohitajika ni wokovu ulio kamili," alisisitiza, akinukuu kitabu cha Waebrania 13:1-6 kinachofundisha kuhusu mwenendo unaomstahili Mkristo aliyeokoka.
Mchungaji huyo alieleza kuwa watu waliookoka wanapaswa kuwa na sura ya maisha inayodhihirisha imani yao.
"Wokovu ni imani, lakini imani za watu wengi sasa ziko chini," alisema mtumishi huyo wa Mungu
Alitaja mambo yanayompasa Mkristo ikiwa ni pamoja na kupendana na kuacha ubaguzi na chuki kuwa wakarimu na kuepuka uchoyo,kujali watu wanaopitia mateso, ndani na nje ya kanisa pamoja na kuridhika na hali ya maisha uliyonayo kwa wakati husika.
"Kesi nyingi za ndoa zinatokana na wanawake kutoridhika na hali ya maisha waliyonayo, Mungu ana wakati wake wa kubariki kila mtu," aliongeza.
Mchungaji Tambikeni amewakumbusha waumini wake kwamba kumpenda Mungu na kuwapenda watu ni msingi wa maisha ya Kikristo.
Hata hivyo amewataka waumini hao kuendelea kumtumainia Mungu, kuwa na moyo wa kujitoa, na kuishi kwa amani na upendo.


Post a Comment