Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito mzito kwa Watanzania kutumia hekima na busara zao wanapojiandaa kuchagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao. Dkt. Samia amesisitiza kuwa uongozi wa nchi unahitaji uzoefu, uthubutu na weledi na haupaswi kupewa kwa mtu yeyote kama eneo la majaribio.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara mjini Bunda, Mkoa wa Mara, Rais Samia alikumbusha umuhimu wa kura kama dhamana ya Taifa. "Kabla hujafanya maamuzi, fikiria kwanza," alisisitiza Dkt. Samia. "Nchi si darasa la majaribio; mpe mamlaka yule unayemwamini ataiongoza kwa hekima na kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa."
Rais alibainisha kwamba kipindi hiki si cha kurudi nyuma au kuanza upya, bali ni cha kuendeleza kasi ya maendeleo iliyopatikana. Alisema Serikali inayoongozwa na CCM imejenga msingi imara katika sekta zote muhimu, ikiwemo elimu, afya, miundombinu, na nishati.
"Tumejenga msingi imara. Tunahitaji kuilinda kasi hiyo kwa kufanya maamuzi sahihi. Kura zetu ndizo nguzo pekee ya kuendeleza amani, umoja, na mafanikio ya taifa hili," alisema Rais huku akishangiliwa na umati wa wananchi wa Bunda. Aliongeza kuwa maendeleo yanayotarajiwa ni matokeo ya uamuzi makini utakaofanywa na kila mpiga kura.
Ziara ya Dkt. Samia, ambayo inaendelea kunadi Ilani ya CCM ya 2025–2030, inalenga kuwashirikisha wananchi katika safari ya kujenga Tanzania yenye ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Rais Samia alisisitiza kwamba Watanzania wanajua thamani ya utulivu na maendeleo. Kura si tu kitendo cha kidemokrasia, bali ni sauti ya uamuzi makini, sauti ya busara, na sauti ya Tanzania yenye matumaini. Alihitimisha kwa kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanatoa kura zao kwa chama pekee kinachoweka maslahi ya wananchi mbele, akisisitiza kuwa chama hicho ni CCM.
Post a Comment