Na Mwandishi Wetu
Kupiga kura si kitendo cha kuweka alama tu; ni msingi wa maamuzi na njia kuu ya kushiriki katika kuamua mustakabali wa nchi.
Ukiangalia historia ya Uchaguzi nchini hasa ule wa Kura Tatu wa mwaka 1958 kwa iliyokuwa Tanganyika, ambapo TANU ilikabiliwa na uamuzi mgumu wa kushiriki au kususia uchaguzi wenye masharti ya kibaguzi, tunapata mafunzo makuu matatu yanayoonyesha umuhimu wa kupiga kura.
Kura ni zana ya kufanya maamuzi ya kimkakati kwa taifa. Katika Mkutano Mkuu wa Tabora, baada ya mjadala mkali, wajumbe wa TANU waliamua mwelekeo wa chama kwa kupiga kura (kura 37 za kuunga mkono kushiriki dhidi ya 23 za kususia). Kitendo hiki kinaonyesha wazi kwamba kura, hata iwe kwa idadi ndogo, ndiyo inakuwa njia ya mwisho ya kuamua hatua ya kisiasa na kwa maamuzi hayo, walifanikiwa, kuleta uhuru wa Tanganyika.
Kura yako, kama kijana, inakuwezesha kuchagua mwelekeo wa serikali na kuamua ni vipi sera zinazoathiri ajira, elimu, na huduma za jamii zitatekelezwa. Kususia kura ni sawa na kutoa mamlaka yako ya kuamua na kukikabidhi chama hasimu ushindi bila wewe kutumia haki yako.
Kura yako inakuwezesha kuchagua mwelekeo wa serikali na nchi. Kama vile kura chache za wajumbe wa TANU ziliamua kushiriki na kuleta uhuru, kura yako inaweza kuamua ni nani na kwa vipi sera zinazoathiri ajira, elimu, na huduma za jamii zitatekelezwa. Kususia kura ni sawa na kukikabidhi chama hasimu ushindi bila jasho, kama alivyosema Mwalimu Nyerere.
Hoja kuu iliyotumiwa na Mwalimu Nyerere na Sheikh Abdallah Rashid Sembe ilikuwa kwamba kususia uchaguzi ingekuwa ni kujiingiza katika mtego wa adui . Walisisitiza kwamba TANU ingedhoofika na ikakosa sauti katika maamuzi ya baadaye ikiwa ingesimama pembeni.
Waliona umuhimu wa kushiriki na kushinda viti ili kupata sauti rasmi ndani ya Baraza la Kutunga Sheria la kikoloni, na hivyo kuondoa mfumo wa Kura Tatu kutoka ndani ya mfumo na walifanikiwa. Kura yako, kwa hiyo, siyo tu hisia bali ni silaha ya kisiasa inayokuwezesha kuzuia wengine wasiamue mustakabali wako. Kwa kupiga kura, unazuia wale usiotaka kuongoza wasipate urahisi, na unawaweka madarakani wale unaoamini wanaweza kutetea masilahi yako.
Kura inalenga kuleta mazingira ambapo viongozi wanachaguliwa kwa idadi kubwa ya wananchi, na hivyo wanakuwa na wajibu wa kujibu matakwa ya wapiga kura wao, hasa vijana ambao ni kundi muhimu la jamii.
"Kiongozi anayejua amechaguliwa na kura yako lazima akusikilize....Hivyo, kupiga kura ni kuhakikisha unachagua watu watakaokutetea na kuweka sera zinazokunufaisha." anasema Mwenyekiti wa Tanzania Bloggters Network Beda msimbe wakati akizungumza katika kipindi cha radio kilichorushwa na Radio Maria hivi karibuni.
Ndio kusema kuna wakati katika historia ya Taifa letu kupiga kura haikuwa haki ya kila mmoja, bali ndoto ya wengi. Leo, kizazi cha vijana kilichozaliwa katika uhuru wa demokrasia kimerithi fursa adimu fursa ya kuchagua, kuamua, na kushiriki katika kujenga mustakabali wa Tanzania.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, alitambua mapema kwamba kura ni zaidi ya karatasi; ni alama ya uhalali wa mamlaka na ishara ya ushiriki wa wananchi katika uongozi wa nchi yao. Hata katika enzi za chama kimoja, tumeshapata uhuru Mwalimu Nyerere alisisitiza wananchi wapige kura kama kipimo cha uungwaji mkono, akiamini kuwa sauti ya wananchi ndiyo msingi wa serikali bora.
“Kura ni tochi ya kuongoza, inatoa nuru ya uhalali, uwajibikaji, na matumaini,” alisema Mzee Juma Hiza (78), mwanahistoria na kuongeza: “Tulikipigania hiki kitambulisho cha kupiga kura. Tuliamini kila raia ana haki ya kusema ‘ndiyo’ au ‘hapana’ kwa amani.”
Mzee hiza anasema kupiga kura ni tendo la shukrani kwa waasisi wetu.Ni uamuzi wa kuthamini uhuru uliopatikana kwa jasho, hekima na ujasiri.p na kuwataka vijana ambao ndio wengi kwenda kuiga kura kwa amani, kwa fahari, na kwa heshima ya waliotutangulia.
Thamini mwanga huu, udumishe kwa ushiriki wako.
Post a Comment