Na Mwandishi Wetu
Tofauti na maneno matupu au hisia za mitandaoni, kura ndio kitendo pekee chenye mamlaka halisi ya kuamua hatima ya Taifa.
Kama Baba Askofu Paulo Bendera, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Dar es Salaam, alivyoshauri, kila mmoja anapaswa kwenda kupiga kura na kumchagua anayemtaka, kwani kususia kura ni sawa na kuchagua hewa—yaani, kukabidhi uamuzi wako kwa wengine.
Viongozi mbalimbali wa jamii wameungana katika wito huu wa amani na utekelezaji wa haki ya kikatiba. Mufti wa Tanzania, ambaye pia ni Shehe Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally amesisitiza suala la amani na kuwaambia vijana wapige kura kama njia ya kuamua hatima yao na kisha warejee katika maeneo yao.
Mufti Zubeir alibainisha kuwa amani ni msingi wa Uislamu, na kila Mwislamu anapaswa kuitetea amani hiyo popote atakapokuwepo.
Kwa upande wake, Joseph Muruta alisisitiza kuwa siasa za amani ni fahari kwa nchi yetu. Naibu Katibu Mkuu wa Kamati ya Amani, Alhajj Othmani Mkambaku, alisisitiza umuhimu wa kura kama haki ya kimsingi na wajibu wa kikatiba.
Alisema, "Lazima Oktoba 29 nijitokeze, ni wajibu wangu kupiga kura kumchagua kiongozi ninayempenda ili aweze kusimamia mambo yetu katika kipindi cha miaka mitano."
Kizazi Kipya: Kura Ni Matokeo, Siyo Jazba
Zikiwa zimesalia siku chache kufikia Uchaguzi Mkuu, kizazi kipya (waliozaliwa baada ya mwaka 2000) kiko tayari kuandika historia yake ya kidemokrasia. Hiki ni kizazi kinachotumia teknolojia kuchambua hoja na kujua ilani, na kura kwao si tukio la kisiasa, bali ni jukumu la kizazi.
Kupiga kura kwa vijana hawa ni ahadi ya kulinda maendeleo, amani, na heshima ya taifa. Wanajua kuwa siasa za maneno matupu au uvurugaji wa mitandao hauwezi kubadilisha hali halisi. Uhalisia unaonekana katika maboresho ya huduma za afya, elimu, na miundombinu—mambo ambayo yanawapa hamasa ya kushiriki.
Kizazi kipya kinajua kwamba kura si kelele; ni matokeo. Ni uamuzi wa kuendeleza yaliyojengwa, kuimarisha yanayobadilisha maisha, na kulinda urithi wa amani wa Tanzania. Taifa hili limejengwa kwenye msingi wa majadiliano, hekima, na umoja. Wale wanaotamani taharuki nje ya mipaka watasubiri bure, kwani Tanzania imara haijengwi kwa fujo, bali kwa umoja wa fikra na sauti za wananchi wake.
Kizazi kipya cha wapiga kura kimeamua. Kitaandika historia kwa kura, si kwa vurugu. Kura zao ni sauti za matumaini, zikiongoza Tanzania katika zama mpya za amani, kazi, na uelewa.
mwisho
Post a Comment