Na Mapuli Kitina Misalaba
Serikali
mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Shirika la CSEMA chini ya ufadhili wa UNFPA
imewakutanisha wajumbe wa kamati ya kusukuma mashauri ngazi ya Mahakama kutoka
ngazi ya Mkoa na Wilaya zote za Shinyanga, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa
huduma za uendeshaji mashauri ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya
watoto.
Akizungumza
wakati wa semina hiyo, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Lydia Kwesigabo, amesema kuwa semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji
wa Mradi wa Haki Yangu, Chaguo Langu, ambao unalenga kuimarisha mpango mkakati
wa kitaifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA)
pamoja na mpango mkakati wa Mkoa wa Shinyanga wa kutokomeza ukatili huo.
“Kupitia
semina hii tumekutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujadili changamoto
zinazojitokeza katika mashauri ya ukatili wa kijinsia na kutafuta njia za
kuyasogeza mbele hadi kufikia hatua ya haki. Pia tunajengeana uwezo na kuongeza
uelewa wa pamoja kwa wataalam wote wanaoshughulika na mashauri haya,” amesema
Lydia.
Ameongeza
kuwa Mradi wa Haki Yangu, Chaguo Langu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya
serikali, UNFPA, CSEMA, na mashirika mengine ya kiraia, ambapo kupitia mikutano
kama hiyo, wadau wanabaini changamoto, kupanga mikakati, na kuimarisha uratibu
wa pamoja katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Kwa
upande wake, Mratibu wa Mradi wa Haki Yangu, Chaguo Langu kutoka Ofisi
ya Kanda ya Shinyanga Bi. Jane Haule, amesema sekta ya Mahakama ina nafasi
muhimu katika kusukuma mbele mashauri ya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha
haki inapatikana kwa wahanga, hasa wanawake na watoto wenye ulemavu.
“Mahakama
ni mhimili muhimu sana wa haki. Ushirikiano kati ya taasisi hizi ni hatua kubwa
katika kuhakikisha kesi za ukatili zinapewa kipaumbele na wahanga wanapata haki
zao kwa wakati,” amesema Jane.
Semina
hiyo imehusisha taasisi mbalimbali zikiwemo:
Mahakama
za Mkoa na Wilaya (Shinyanga, Kishapu na Kahama), Ofisi ya Mashtaka, Ofisi ya
Mganga Mkuu wa Mkoa na Wilaya, Idara ya Ustawi wa Jamii Mkoa na Wilaya, Jeshi
la Polisi (RCO, OC CID – Kahama na Kishapu, pamoja na Dawati la Jinsia), TAKUKURU,
Uhamiaji, Magereza, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii, Probation Officer
Semina
hiyo ya siku mbili inalenga kutathmini changamoto na mafanikio katika
uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto, sambamba na
kuandaa mpango kazi wa pamoja utakao saidia kuboresha uratibu wa taasisi hizo.
Baadhi
ya washiriki wamepongeza CSEMA kwa uratibu mzuri wa semina hiyo na kuahidi
kutekeleza kwa vitendo maazimio yote yatakayofikiwa, ili kuhakikisha
upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga.

Mratibu wa Mradi wa Haki Yangu, Chaguo Langu kutoka Ofisi ya Kanda ya Shinyanga Bi. Jane Haule, akielezea umuhimu wa sekta ya Mahakama hasa katika kusukuma mashtaka kuwa sehemu ya kuunga jitihada za upatikanaji wa haki kwa kesi za masuala ya unyanyasaji wa kijinsia hususan zinazohusu wanawake na Watoto wenye ulemavu.

Post a Comment