Mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amefanya mikutano yake ya kampeni
mkoani Shinyanga, akiwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuiongoza nchi kwa kipindi
kingine cha miaka mitano ili aweze kukamilisha na kusimamia miradi ya maendeleo
iliyoanzishwa katika uongozi wake wa awali.
Dkt. Samia amewasili mkoani Shinyanga asubuhi akitokea
wilayani Maswa, ambapo ameanza ziara yake ya kampeni kwa kuzungumza na wananchi
wa maeneo mbalimbali, akiahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili
wachimbaji wadogo na sekta nyingine za uzalishaji endapo ataendelea kuaminiwa
na wananchi.
Amesisitiza kuwa lengo la serikali ya awamu ijayo
litakuwa ni kuimarisha, kulinda na kuheshimu utu wa Mtanzania kupitia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoainishwa katika ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Katika hotuba yake, Dkt. Samia amesema serikali yake
itaendeleza kasi ya ujenzi wa miundombinu, hususan katika barabara, elimu, afya
na maji, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora na fursa za
kiuchumi.
Kwa upande wao, wagombea ubunge wa majimbo ya
Shinyanga, akiwemo Paschal Patrobas Katambi na Azza Hillal, wamemshukuru Rais
Samia kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika mkoa huo, hasa katika miradi ya
miundombinu na huduma za kijamii.
Wamesema juhudi hizo zimechochea uwekezaji mpya na
kuinua uchumi wa wananchi katika sekta mbalimbali.
Dkt. Samia ametamatisha kampeni zake mkoani Shinyanga kwa
mkutano katika wilaya ya Kahama, kabla ya kuelekea mikoa mingine na kwamba kampeni
za uchaguzi huo zilianza Agosti 28, 2025 na zinatarajiwa kumalizika Oktoba 10,
2025, siku moja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba 11, 2025.

Post a Comment